Na Dk. Reubeni Lumbagala, JamhiriMedia, Dodoma
Utunzaji wa mazingira ni jukumu letu sote. Uwe mtoto, kijana, mtu mzima au mzee. Uwe mwanamke au mwanamme, uwe msomi au usiwe msomi, suala la utunzaji mazingira linakuhusu.
Faida za utunzaji mazingira zinatunufaisha sote. Madhara ya uharibifu mazingira yanatuathiri sote. Hakuna aliye salama mazingira yakiharibika. Ndiyo maana ni vyema mikakati ya utunzaji mazingira ikafanyika mapema.
Dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Kutokana na changamoto hiyo, mikakati inawekwa ya namna bora ya kukabiliana na changamoto hiyo ili kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi na kufurahia maisha.
Tanzania kwa kuwa si kisiwa, tumeathirika pia na mabadiliko ya tabianchi kama zilivyo nchi nyingine. Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo suala la kuhamasisha watu binafsi, taasisi, makampuni na wizara kupanda miti ili kupunguza athari.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa mfano mzuri wa kuigwa kuanzia kuhamasisha watu kupanda miti hadi kufanya kwa vitendo yeye mwenyewe kupanda miti. Tangu akiwa Makamu wa Rais, Dk. Samia kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira hadi sasa amekuwa Rais kamili, anaendelea kuhimiza sana utunzaji mazingira na kupanda miti kwa maendeleo.
Hata katika kuadhimisha Siku yake ya kuzaliwa (Birthday) Januari 27, 2026, Rais Samia aliitumia siku hiyo kupanda miti. “Sisi tulirithi uoto wa asili mwingi sana, tulirithi nchi yetu ambayo haikuwa imeharibika kiasi hiki.
Tulirithi miti mingi ya matunda iliyopandwa shambani na mingine kujiotea. Lakini leo mtoto wetu akitaka kula pera lazima akalinunue sokoni. Sisi tulikuwa tunapita msituni na kula mapera ya aina yoyote tunayotaka,” amesema Rais Dk. Samia.
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kama taasisi ya elimu iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nayo imeunga mkono juhudi za kutunza mazingira kwa kuweka mpango wa kupanda miti ipatayo 150,000 katika taasisi mbalimbali za elimu kama shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu nchi nzima.
Machi 18, 2026, Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Mohamed, alizindua zoezi la kitaifa la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Makutupora ya Jijini Dodoma ambapo katika shule hiyo, miti 600 imepandwa kufuatia agizo ya Rais Dk.Samia kwa NECTA katika maadhimisho ya miaka 50 ya NECTA. Prof Said amesema “Desemba 16, 2023, Rais Dk. Samia alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka miaka 50 ya NECTA alitupa maagizo ya kupanda miti kwa sababu sisi ni watumiaji wa karatasi ambazo zinazalishwa na miti, hivyo tunapanda miti kuunga mkono jitihada za utunzaji mazingira.”
Mkakati wa NECTA wa kupanda miti 150,000 katika taasisi mbalimbali za elimu utachangia kwa kiasi kikubwa jitihada za kuiokoa nchi yetu na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Lakini pia miti hiyo itasaidia kupendezesha mandhari za shule na vyuo na kufanya sehemu hizo kuwa vutivu kwa ufundishaji na ujifunzaji wa maarifa, stadi na ujuzi.
Hakika nawapa kongole NECTA kwa kuratibu mkakati huu mzuri wa kupanda miti katika taasisi za elimu. Kwa mwaka 2023/2024, NECTA walipanda miti 82,676, mwaka 2024/2025 walipanda miti 110,400 na kwa mwaka 2025/2026, lengo ni kupanda miti 150,000. Muhimu ni wanufaika wa shule zitakazopata miche ya miti, kuitunza kikamilifu miti hiyo kwa manufaa endelevu.
Maoni 0620 800 462.





