Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile (Mb), ameielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha inasimamia kwa karibu na kwa uthabiti miradi yote ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa miradi yenye viashiria vya rushwa haipaswi kuendelea kwa kuwa inarudisha nyuma juhudi za Serikali na matarajio ya wananchi.
Akizungumza Juni 19, 2025, mara alipotembelea kwenye banda la maonesho ya Taasisi hiyo kwenye Maonesho yanayoendelea ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Kihenzile ameipongeza TAKUKURU kwa kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo kwa kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kurubuniwa na wanasiasa wanaotumia rushwa kama ngazi ya uongozi.

“TAKUKURU hakikisheni mnatoa elimu muhimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutoa na kupokea rushwa,muwaelimisha ili wasikubali kuchagua viongozi wanaotoa rushwa kwa sababu viongozi wa aina hiyo hawawezi kuleta maendeleo ya kweli,” amesema Kihenzile.
Aidha, ameeleza kuwa rushwa kwenye utekelezaji wa miradi ya Serikali ni sumu kwa maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa TAKUKURU ina jukumu la kuhakikisha fedha za umma zinalindwa na miradi yote inatekelezwa kwa uadilifu, uwazi na kwa viwango vinavyotakiwa.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, TAKUKURU hakikisheni mnasimama vyema kwenye nafasi yenu ili taifa lipate viongozi waadilifu na miradi ya maendeleo isibaki kuwa chanzo cha watu kujinufaisha binafsi,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uelimishaji Umma – TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Faustine Malecha, amesema taasisi hiyo inatumia maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kuhusu athari za rushwa kwenye uchaguzi na utekelezaji wa miradi ya umma.
“Tunahakikisha wananchi wanajengewa uelewa juu ya haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi bora bila kushawishiwa kwa rushwa, kwani chaguo la viongozi kwa misingi ya hongo hudhoofisha maendeleo ya jamii nzima,” amesema Malecha.
Amesisitiza kuwa Taasisi yake imejipanga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa karibu zaidi, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo haigeuki kuwa mwanya wa kujipatia utajiri wa haramu.

“Tutashirikiana na Wananchi kuhakikisha kuwa kila hatua ya utekelezaji wa miradi inazingatia sheria, kanuni na maslahi ya taifa,” amesema
Pamoja na Mambo mengine Wiki ya Utumishi wa Umma imeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za Serikali kutoa huduma, kuelimisha wananchi, na kuonesha uwajibikaji katika utendaji wa kila siku.
Ushiriki wa TAKUKURU katika maonesho hayo umeweka msisitizo mkubwa kwa mapambano dhidi ya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu 2025.
