Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa uamuzi wa kujiondoa kwa mfadhili wao mkubwa Marekani kutatingisha pakubwa miradi ya kiafya ya shirika hilo la umoja wa mataifa.

Mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus ametoa wito kwa mataifa mengine yaendelee kuchangia ili miradi ya kiafya inayowahudumia wengi wa walio maskini duniani isiporomooke.

“Twafahamu kuwa wafadhili wana uhuru wa kuamua wapi na kwa akina nani wanataka kutoa fedha zao kuchangia miradi mbalimbali yaani kwa jumla wana uhuru wakutumia fedha zao watakavyo na tunashukuru kwa wale waliosaidia kufadhili miradi ya kiafya duniani lakini kinachotutatiza ni maamuzi yanayofanywa ghafla ya kukata misaada hiyo na wakati huo huo kunafanyika mabadiliko makubwa ya mifumo ya kiuchumi na kibiashara hali hiyo inavuruga pia sekta hii muhimu ya afya ya umma.” alisema.