Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Mwanza

Ndugu zangu Watanzania, taifa letu linaelekea katika moja ya hatua muhimu za kidemokrasia – Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025. Hii ni siku ambayo wananchi tutatumia kalamu na karatasi kuamua mustakabali wa nchi yetu kwa miaka mitano ijayo. Ni siku ya kihistoria, lakini pia ni siku inayohitaji busara, utulivu na umoja.

Sitanii, Tanzania tumebarikiwa kuwa miongoni mwa mataifa machache barani Afrika yaliyodumisha amani kwa zaidi ya nusu karne tangu tupate uhuru mwaka 1961.

Tumefanya uchaguzi mara nyingi. Kubwa la kujivunia kila tulipomaliza uchaguzi, tumebaki ndugu, majirani na Watanzania wa taifa moja. Hata hivyo, kila uchaguzi huibua hisia kali, maneno makali na wakati mwingine chuki zisizo za lazima.

Uchaguzi ni sehemu ya mchakato wa kisiasa, si mwisho wa maisha. Baada ya kura kupigwa na matokeo kutangazwa, maisha yataendelea. Watoto watarudi shuleni, wafanyabiashara wataendelea na shughuli zao, wakulima watarudi mashambani, na watumishi wa umma wataendelea kuhudumia wananchi. Tanzania haitasimama kwa sababu chama fulani kimeshinda au kimeshindwa.

Sitanii, nazisikia sauti zinazotoka ughaibuni zaidi kuliko za ndani. Zinahamasisha Watanzania kuandamana. Kufanya vurugu. Sauti hizi zinatuchochea tugawanyike. Wapo baadhi ya wanasiasa na watu wenye masilahi binafsi wanaotumia chaguzi kama fursa ya kuwachochea wananchi kwa masilahi yao binafsi.

Wanatupa maneno matamu, wanatengeneza hofu na kutumia mitandao ya kijamii kusambaza chuki. Wakati mwingine wanawafanya vijana kuwa askari wao wa mitaani.

Ni muhimu tuelewe kuwa demokrasia si vita, bali ni mashindano ya hoja na sera. Kila chama kina haki ya kueleza sera zake, na wananchi wana haki ya kuchagua. Vyombo vyenye jukumu la kusimamia uchaguzi navyo vina wajibu. Nianze na Tume  Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Tume hii ina wajibu wa kuhakikisha haki si tu inatendeka, bali ionekane mbele ya macho ya watu kuwa imetendeka.

Mchakato wa kugawa vifaa vya kupigia kura tunategemea uende kwa uwazi. Hatutarajii kusikia vifaa vimechelewa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura. Wimbo uliozoeleka ambao umekuwa chanzo cha vurugu miaka yote wa mawakala kunyimwa fomu za viapo, tunaamini mwaka huu hautajitokeza.

Sitanii, mwaka huu tumeshuhudia kampeni zenye ustaarabu wa hali ya juu. Vyama vimejielekeza katika hoja za jinsi gani vikishinda vitakavyowahudumia wananchi. Vimeahidi huduma bora katika sekta ya elimu, afya, maji, miundombinu, utawala bora na nyingine nyingi. Vyote vimeahidi vikishinda maisha ya wananchi yataimarika pia.

Nikiri, ni uchaguzi pekee ambao hadi sasa hatujasikia bomu la machozi likipigwa au wagombea kushushwa majukwaani kwa kukaidi muda uliokubaliwa wa saa 12 jioni. Ni uchaguzi pekee pia ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeususia kwa kusema hakuna mabadiliko yaliyofanyika. Hata kama serikali imetunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na nyingine.

Sitanii, Tanzania ni yetu sote. Rais atakayechaguliwa ni wa Watanzania wote, si wa chama chake pekee. Wapinzani watabaki kuwa sauti muhimu ya kuikosoa serikali kwa nia ya kujenga, si kubomoa. Vyombo vya habari, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuendeleza majadiliano ya kujenga taifa, si kubomoa.

Baada ya Oktoba 29, tutabaki majirani, marafiki na ndugu. Tutaendelea kuhudhuria harusi na kushirikiana katika matukio ya kijamii. Ni kwa minajili hiyo nasema, tusiruhusu tofauti za kisiasa zitugawanye. Uchaguzi ni tukio la muda mfupi, lakini amani ni urithi wa kudumu.

Watanzania tumeilinda amani yetu kwa muda mrefu. Tusiiuze kwa hasira za muda mfupi, bila kujipa muda wa kutafakari tulikuwa wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi.

Ujumbe hasa kwa vijana ni kuwa tukilinda amani, tutakuwa na nafasi ya kuijenga Tanzania yenye matumaini kwa wote, ya sasa na ya baadaye. Tujiepushe na vurugu, tuchague kwa amani, tusiwasikilize walioshiba wakiishi ughaibuni na tukumbuke – kuna maisha baada ya uchaguzi.

Mwisho, wakati nawatakia heri Watanzania katika uchaguzi huu, sikutaka kurejea ahadi zilizotolewa katika uchaguzi. Jambo moja lililogusa moyo wangu ni ahadi ya kutafuta maridhiano baada ya uchaguzi ndani ya siku 100. Tukae tuulizane. Tulikosea wapi, tumepatia wapi na tufanye nini tusikosee tena, ikiwa tulikosea. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827