Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaounda kundi la G55 , wametangaza kuondoka ndani ya chama hicho kwa kile walichoeleza kuwa kushindwa kutokana na kutengwa kwa kuwa walimuunga mkono Freema Mbowe wakati wa chaguzi

Hayo yamebainishwa leo Mei 7, 2025 wakati wakizugumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Wamedai tangu uongozi wa Tundu Lissu uingie madarakani kumekuwa na ukiukwaji wa katiba jambo ambalo wamesema hawataweza kulivumilia.

Wanachama hao ni Catherine Ruge, Salum Mwalimu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Julius Mwita, John Mrema pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila.

“Hivi sasa CHADEMA imegubikwa na ubaguzi mkubwa dhidi ya wanachama wanaohusishwa na upande wa Freeman Mbowe, ambao wamekuwa wakitengwa kuanzia ngazi ya kamati Kuu hadi mashinani vitendo hivi niukiukwaji wa katiba.

“Baada ya kumalizika kwa chaguzi Mbowe alitoa wa kuvunjwa kwa makundi na kuundwa kwa kamati ya maridhiano baada ya uchaguzi wa chama lakini ushauri huo uligonga mwamba mara moja mbele ya wajumbe na umeendelea hadi sasa” amesema Catherine.

Catherine amesema kuwa wakati Mbowe akizugumza baada ya uchaguzi, alitoa ushauri kwenye chama kuvunja makundi na kukiunganisha chama na kuunda kamati ya maridhiano ili chama kiweze kurudi pamoja kupigania haki, utu na maendeleo ya watu. Lakini mwenyekiti aliyeshinda alimshutumu Mbowe palepale mbele ya wajumbe.

“Leo CHADEMA niliyoitumikia kwa jasho langu la damu ndani ya miaka 15 na hakuna anayeweza kubeza, badala ya kubuni mbinu ya kuwapa matumaini wananchi namna ya kuikabili CCM matokeo yake wanawatia hofu Watanzania” amesema.

Naye Kigaila amesema kuwa vitendo hivyo vya ubaguzi vimeendelea kwa wanachama wanaojulikana kuwa walimuunga mkono Mbowe, ambao sasa wanatengwa waziwazi.

“Hivi sasa kil anayejulikana kwamba alimuunga mkono Mbowe anaitwa msaliti. Hali hii imeenea kuanzia Kamati Kuu hadi kwenye misingi ya chama.

“Sisi tumeamua wote pamoja kujiondoa CHADEMA ili tuwaachie waendeshe wanavyotaka. Sisi hatuwezi kuwa wanachama wa chama ambapo uamuzi wake haufanywi kwa vikao, hatuwezi kuwa wanachama ambao tunabaguliwa, katiba haifuatwi” amesema Kigaila.

Hata hivyo amesema kuwa wanafanya mawasiliano na vyama mbalimbali ili kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa sababu bado hawajazeeka” Tunaondoka leo CHADEMA tunaenda kutafakari tutaenda chama gani, lakini mjue CCM si mbadala wetu ila tutawaambia ni wapi tunakwenda.”

Naye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Zanzibar, Salum Mwalimu amesema anaungana na wenzake kukihama chama hicho kwa kuwa kila wakijaribu kuushauri uongozi uliopo hoja yao ni No reforms, no election hawasikilizwi badala yake wanaendelea kubaguliwa na kutoshirikishwa kwa jambo lolote.

Ameongeza kuwa yeye amekaa CHADEMA miaka 17, lakini kila anapotoa ushauri wa jambo hasikilizwi “Sisi ni watu wazima, tumevumilia tumechoka ndani ya CHADEMA hakuna kinachoendelea.

“Kwenye vikao wamekuwa wanaangaliana wewe ni No reforms, no election, kama si mlengo huo unatengwa, haiwezekani tubaki CHADEMA kwa mazingira ya namna hiyo,” amesema

Ameongeza kuwa uongozi uliopo madarakani una udhaifu na ndio maana chama kinaendeshwa kwa matamko na hawazungumzi lugha moja.

“Natangaza rasmi uanachama wangu ndani ya CHADEMA unakoma, hakuna cha kuogopa naenda kuendeleza taranta yangu sehemu nyingine,” amesema Mwalimu.