Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Kibaha

MWENYEKITI wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, amesema vyombo vya dola vimejipanga kuhakikisha hali ya usalama inakuwa shwari na hakuna yeyote atakayebughudhiwa au kutishwa wakati wa mchakato wa upigaji kura.

Amesema kamati ya usalama imeweka mikakati madhubuti na ina taarifa za kina kuhusu hali ya kila eneo la mkoa, hivyo wananchi wanapaswa kuwa watulivu na kutoingiwa na hofu.

Akizungumza na wananchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, Kunenge alitoa onyo, wamejipanga na anasisitiza hakuna mwananchi atakayenyimwa haki yake ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi.

Kunenge, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alisema maandalizi ya uchaguzi yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha, na Tume Huru ya Uchaguzi imeweka vituo 3,941 vya kupigia kura ili kusogeza huduma hiyo karibu zaidi na wananchi.

“Nawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupiga kura,” alisema Kunenge.

 “Chagueni viongozi watakaoweza kutatua changamoto zenu na kuwaletea maendeleo, kulingana na sera zilizowasilishwa na vyama vyao.”

Alisema serikali imefanya maandalizi ya kutosha, ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi na makundi mbalimbali kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi kwa amani.

Katika hatua nyingine, Kunenge alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza siku ya uchaguzi kuwa mapumziko rasmi, ili wananchi wote wapate fursa ya kushiriki katika zoezi hilo la kitaifa.

Alifafanua kuwa vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, na kwamba wananchi watakaokuwa bado kwenye foleni muda wa kufunga vituo utakapowadia, wataruhusiwa kupiga kura hadi wote watakapomaliza.