Kwanza naungana na familia, ndugu na Watanzania wote katika kuomboleza msiba uliotufika wa kufiwa na mzazi wetu, ndugu yetu, rafiki yetu na kiongozi wetu mpendwa, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi, wiki iliyopita. Inna Lillahi Wainna Ilayhi Raajiuun.

Mauti ni faradhi na kila nafsi itaonja. Alhaj Aboud Jumbe ni baba yetu, ndugu yetu na kiongozi wetu tuliyempenda, tuliyemthamini na tuliyemheshimu si kwa haiba yake wala kwa ukarimu wake tu, bali na uadilifu wake, unyenyekevu wake na adabu zake mbele ya kila mtu. Kwa tabia hii ilimpa daraja kubwa la kutiiwa na kufuatwa. Yote hayo sasa hayapo.

Marehemu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi alikuwa kiongozi bora kati ya viongozi adhimu nchini na mwanafalsafa mtiifu aliyeamini na aliyemcha Mwenyezi Mungu (Allah) usiku na mchana.

Hakika katika umri wake wa miaka 96 duniani, alitafuta amali njema ya dunia na amali njema ya akhera. Aboud Jumbe ninayemfahamu, haikuwa rahisi kwake kuugawa mwili na akili zake, nusu mambo ya anasa na nusu mambo ya dini. Yeye alikuwa mwili mzima muumini wa Uislamu na aliyesimamisha swala.

Ewe Mola wetu tunakuomba mpokee mja wako na umlaze mahali pema peponi hadi siku ya hesabu. Amin. Nasi tulio hai duniani tufuate mwenendo wake na kumtakia rehema kwa Muumba wake. Insha’allah.

Kifo cha Alhaj Jumbe kimetoa mshtuko kwa Watanzania. Hilo ni jambo la huzuni kuondokewa lau kama ni la kawaida. Lakini watu hutaharuki kwa vile kifo hakina huruma wala hakizoeleki na hakina rafiki. Kinapotokea watu hurudi na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusahau hitilafu zilizopo kati yao.

Nisingependa kurudia kueleza wasifu wake marehemu enzi za uhai wake duniani katika maisha, uongozi na huduma kwa Watanzania kuanzia kwenye michezo, siasa hadi serikalini, kwa sababu waandishi wengi wameshazungumzia tangu afariki dunia, ila naona heri kusema yafuatayo:

Binafsi nimesikitishwa na kuhuzunika kusikia katika vyombo vya mawasiliano kuwa wakati wa maziko  yake,  kiongozi ninayemheshimu, Maalim Seif Shariff Hamad, amekataa kupokea mkono wa tanzia heri na amani uliotolewa na Rais wa Zanzibar, Dakta Ali Mohamed Shein.

Nasema nimesikitishwa nikiamini Maalim Seif, Dakta Shein na marehemu Alhaj Jumbe ni ndugu katika Uzanzibari wao na Uislamu wao. Wote wanazungumza tamko moja la Uislamu ni amani. Vipi Maalim Seif ukatae kupokea amani iliyo ndani ya dini yako kwa maelezo ya Mtume Muhammad (S.A.W)?

Kukataa kupokea mkono wa amani na kuonesha kisirani mbele ya umati ni kumkataa Mtume Muhammad (S.A.W) Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Vipi walipa tendo la dunia la matakwa binafsi cheo badala ya ibada? Mtume Muhammad (S.A.W.) hakuagiza hivyo kwa ndugu Waislamu.

Nakuomba kiongozi wangu matendo kama hayo usiyape kipaumbele yanakuchafulia. Ni vyema kutakiana amani kama dini zinavozungumza. Naamini ile dhana ya kuhudhuria maziko ya kiongozi wako umeitia dosari.

Maalim Seif, marehemu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi ni mwalimu wako, mkuu wako wa kazi na kiongozi wako wa nchi, ambaye amekupa ushauri na maelekezo kuhusu uongozi na kusamehe. Vipi leo unajaa kisirani wakati wa maziko yake? Je, Dkt Ali Mohamed Shein si mwenzako, swahiba wako?

Baadhi ya ndugu zako wanasema (wimbo ‘Mpewa hapokonyeki), aliyepewa kapewa, wewe ukifanya chuki, bure unajisumbuwa.

Aliyepewa kapewa, naapa hapokonyeki, kwa alichojaaliwa, wallah hapunguziki kwake ukiliya ngoa, bure unajipatisha dhiki, wa tisa humpa tisa, wa moja haongezeki, alomnyima kabisa pindi akitaharuki, Mola mtoa hidaya, mambo yote kamiliki kwa unomturukiya, huwa ndiyo yake haki na asije mtakiya, huwa si yake kaini.

By Jamhuri