
Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Mikumi
Naandika makala hii nikiwa safarini kuelekea Ifakara. Jumamosi, Machi 28, 2026 nimepata fursa ya kushiriki mazishi ya kitaifa ya kaka na ndugu yangu, William Vangimembe Lukuvi.
Nikiri nilimfahamu Lukuvi mwaka 1993, na hasa kuanzia mwaka 1994 alipochaguliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba. Hii ni wilaya yangu ya nyumbani nilipozaliwa.
Sitanii, sifa nyingi za Lukuvi zimeelezwa. Ipo moja ambayo haikuelezwa sawia. Lukuvi ni kiongozi pekee katika historia ya siasa za Tanzania aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, akawa Waziri, akawa Mkuu wa Mkoa, akarejea kuwa Waziri, akatenguliwa, akawa mshauri wa Rais, akawa tena Waziri.
Ni waziri pekee aliyepata kuwa Mnidhamu wa Serikali Bungeni mara mbili. Wengine wanaanzia ukuu wa wilaya, wanakuwa wakuu wa mikoa, na ni wachache kupitia kada hii wanaochomoza kuwa mawaziri, ila wapo.
Mambo mawili niyagusie. Kati ya kazi nyingine nilizofanya naye zipo mbili nisizozisahau. Mwaka 2009 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria, nilihariri tasnifu (research paper) yake, ambapo alitafiti hali ya siasa Zanzibar, hasa eneo la Pemba.
Utafiti huu ulimwezesha kupata shahada ya uzamili. Utafiti huu niliuhariri ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo yangu ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Hull, nchini Uingereza.
Tuliendelea kufanya kazi kwa karibu na Lukuvi, ambapo tukio la pili ninalogusia ni la mtu aliyejiita mwekezaji alipovamia Kijiji chetu cha Nyanga, wilayani Bukoba, akadai kuwa uongozi wa kijiji, awali ulimuuzia ekari tano katika eneo la Kyankorongo, lakini baadaye akaongezea malipo akauziwa kijiji chote!
Mwekezaji uchwara huyu, aliwafungulia kesi viongozi wa kijiji na wanakijiji zaidi ya 40, akiwadai fidia ya Sh bilioni moja. Alikuwa anawapiga watu makofi na kuwatishia kwa bunduki. Nilipopata taarifa, nikafuatilia na kubaini mambo mawili.
Kwanza, huyo mwekezaji alikuwa ameghushi hati ya ardhi. Idadi ya ekari alizozitaja zilikuwa zinachukua eneo lote la Kitongoji cha Nyanga, linajumuisha mitaa ya Kyakailabwa, Kyamyosi na Rubumba zinazounda Kata ya Nyanga, badala ya ekari tano alizopewa.

Sitanii, ukubwa wa eneo kwenye hati aliyokuwanayo, vipimo vilionyesha hata kata za Kagondo na Buhembe ilibidi zichukuliwe kutimiza eneo alilodai ni lake. Nilibaini pia kuwa huyo mwekezaji alikwishaukana Utanzania na kupata uraia wa Uingereza.
Yote haya nilimpatia Lukuvi kama taarifa za kusaidia kufanya uamuzi. Aliunda Kamati Maalumu mwaka 2018. Alibaini ukweli wote.
Baada ya kupata ukweli, akaniambia tukutane Bukoba. Nilisafiri tukakutana eneo la Chemba. Katika mkutano huo alinipatia nafasi ya kueleza kero hii. Alimwita huyo mwekezaji akamuuliza: “Wewe ni Mtanzania?”
Kwa tambo huyo jamaa akajibu: “I’m British (Mimi ni Mwingereza)!” Alimhoji ukubwa wa eneo unaoonekana kwenye hati kama unalingana na uhalisia wa eneo ardhini, akainama.
Kilichofuata baada ya hapo ni historia. Lukuvi alielekeza huyo mwekezaji akamatwe na kufukuzwa nchini. Kumbe alikuwa na maeneo mengine anafuga ng’ombe! Hata kwenye mbuga za wanyama.
Aliamuru afikishwe mahakamani mara moja na kufukuzwa nchini kwani si raia wa Tanzania. Muda huohuo mwekezaji huyo akatiwa pingu, akapandishwa kwenye ‘difenda’ nyuma akiacha Prado lake na kunyang’anywa ‘mguu wa kuku’ aliokuwa nao kiunoni.
Sitanii, tukio hili lilishangiliwa na kuwafanya watu wampende Lukuvi kupita kiasi. Hadi alipofariki dunia, viongozi wa kijiji akiwamo Diwani wa Nyanga, Stephen Ngaiza, alinipigia simu kusema wana-Kata ya Nyanga wanamwombea Lukuvi Mungu amlaze mahala pema peponi, maana kama si yeye, huyo mwekezaji alikuwa tayari ametangaza kuwa angejenga uzio kuzunguka kijiji.
Akasema angeweka geti ambalo wakazi wote wangeingia au kutoka katika Kijiji cha Nyanga kwa kujiandikisha kwenye kitabu maalumu asubuhi na jioni. Haifikiriki. Kwaheri Lukuvi. Tutakukumbuka kwa kumaliza kero hii.
Kifo cha Lukuvi kimeacha huzuni nzito mioyoni mwa Watanzania. Ni huzuni ya kumpoteza kiongozi aliyepitia misukosuko mingi ya siasa za nchi hii, aliyebeba kumbukumbu za nyakati ambazo siasa zilikuwa na mipaka ya heshima, subira na utaratibu.
Lukuvi hakuwa mkamilifu, lakini alisimama kama alama ya kizazi kilichoamini kuwa uongozi ni safari ya maandalizi, si mbio za ghafla.
Sitanii, wakati taifa likiomboleza, kuna jambo linatisha zaidi kuliko msiba wenyewe – kelele za chini kwa chini za kuanza mbio za urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.
Ni mapema mno. Si mapema tu, bali ni hatari. Historia yetu ipo wazi kama kioo. Mwaka 1984, kilichompata Aboud Jumbe Mwinyi akiwa Rais wa Zanzibar, ni vigumu kukitenganisha na mbio za urais za mwaka 1985.
Halikuwa tukio la kawaida la kisiasa. Ilikuwa ni mwanzo wa nyufa ndani ya mfumo wa uongozi. Uamuzi ule uliweka mbegu ya sintofahamu iliyokuja kujidhihirisha miaka michache baadaye – upepo wa mageuzi ya vyama vingi mwaka 1992 ulipoanza kuvuma. Hapo ndipo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilianza kukutana na changamoto halisi ya ushindani.
Mwaka 1995, matokeo yake yakawa dhahiri. Agustino Lyatonga Mrema alisimama kama tishio la kweli kwa CCM. Ilikuwa ni ishara kwamba wananchi wanapohisi kuna migawanyiko au ubabe wa ndani, huanza kutafuta njia mbadala. Lakini bado hatukujifunza vya kutosha. Hapa sitazungumzia kundi la G55 lililoongozwa na akina Njelu Kasaka!
Mwaka 2012, kaulimbiu ya ‘kujivua gamba’ iligeuka kuwa uwanja wa mapambano ya ndani, ilizaa mpasuko mkubwa. Wanasiasa wakubwa kama Edward Ngoyai Lowassa walijikuta katikati ya mgogoro ulioitikisa CCM.

Na mwaka 2015, tulishuhudia upinzani ukipata nguvu isiyokuwa ya kawaida kutokana na mpasuko huu, hali iliyoonyesha wazi kuwa migawanyiko ya ndani ya chama tawala ni zawadi kwa wapinzani wao.
Mwaka 2020, mbinyo wa kisiasa ulizidi kujitokeza. Na matukio ya Oktoba 29, 2025 – yaliyoacha maswali mengi katika jamii – yanapaswa kuwa kengele ya tahadhari kwamba mvutano wa kisiasa unapofikia kiwango fulani, huathiri siasa, jamii na hata imani ya wananchi kwa mfumo mzima.
Sitanii, dunia ya leo si ya jana. Kuna nguvu mpya ambayo haiwezi kupuuzwa – mtandao na mitandao ya kijamii. Habari haisafiri tena kwa kasi ya magazeti au redio pekee; sasa ni sekunde chache tu, mjadala unakuwa wa kitaifa. Na zaidi ya hapo, kuna kizazi kipya cha vijana – wenye ndoto, wenye hasira, na wenye matarajio makubwa ya maisha bora.
Hawa vijana wamejengewa matumaini makubwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050). Wamehamasishwa kuhusu uchumi imara, ajira, ubunifu na maendeleo jumuishi kupitia Dira 2050. Sasa wanasubiri kuona hayo yakitekelezwa. Je, wataelewaje pale viongozi wanapoanza mapema kuzungumzia nani atakuwa Rais mwaka 2030 badala ya kujadili namna ya kufikia malengo ya Dira 2050?
Hili ndilo kosa kubwa linaloweza kufanyika sasa. Kwa CCM na kwa wanasiasa wote kwa ujumla, huu si wakati wa kupimana nguvu za urais wa baadaye. Huu ni wakati wa kupimana uwezo wa kuleta maendeleo ya sasa kwa maendeleo ya watu wetu. Wananchi hawahitaji mijadala ya majina ya wagombea; wanahitaji majibu ya changamoto zao – ajira, bei za bidhaa, huduma za jamii na mustakabali wa watoto wao.
Sitanii, nikiuliza swali hapa, sijui jibu lipi mtanipa. Hivi mlipata kuwaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliandaliwa na mfumo kupata uzoefu na ujuzi wa uogozi bila yeye kujua hadi akafikia kuwa Rais wa Tanzania? Mnaona Rais Samia anaepuka kuwa na makundi kutokana na kwamba kabla ya kuwa Rais alijikuta anafanya kazi na kila mtu, bila kuanza mbio mapema ambazo zingemtengenezea maadui?
Kwa hakika, siasa za mapema ni sumu ya utulivu wa kisiasa. Zinazaa makundi, zinachochea fitina, na zinapunguza muda wa serikali iliyopo madarakani kushughulikia maendeleo ya watu, badala yake watumishi ndani ya serikali wanabaki kutafutana, kupigana fitina na majungu, huku muda wa kutumikia wananchi ukipita bila kufahamu. Mwishowe, anayepoteza si chama tu – ni taifa zima.
Kifo cha Lukuvi kinapaswa kuwa somo. Somo la utulivu, subira na kuheshimu nyakati. Kama kweli tunamuenzi, basi si kwa maneno ya rambirambi pekee, bali kwa kurejesha nidhamu ya kisiasa aliyoiwakilisha, basi tuache mbio za 2030.
Tujadili Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kila kona – ndani na nje ya CCM. Tujadili namna ya kuboresha maisha ya watu, si namna ya kugawana madaraka ya kesho.

Sitanii, naomba nihitimshe na jambo moja. Ebu kila Mtanzania aridhike na nafasi aliyonayo. Mimi Balile nikiwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI, nimshukuru Mungu kwa wadhifa na fursa hiyo niliyonayo. Nisiwe na husuda, wala hiyana.
Nisitamani mali ya mtu mwingine. Tukiridhika na tuliyonayo, tutatumikia uadilifu na utiifu na kazi zote zitakwenda kwa furaha, maendeleo tutayaona.
Umoja wetu ni zaidi ya utabiri wa nani atakuwa Rais mwaka 2030. Nikidurusu historia ya taifa letu na mawimbi ya kuusaka urais, napata hofu. Nimezisikia kauli kuanzia kwenye minong’ono, lakini sasa zipo kweye majukwaa ya kisiasa hadi Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee Stephen Wassira, amekemea mbio za mapema za urais.
Napata hofu kuwa tunarudia historia ile ile, kwa gharama kubwa zaidi. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827

