Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti Usafirishaji Ardhini (LATRA) imesema kuwa itaendelea kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za usafiri salama na nafuu.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.
Amesema kuwa mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha mifumo ya usafiri nchini inakidhi viwango vya ubora na usalama, sambamba na kulinda maslahi ya wananchi.
Amesema ushiriki wa LATRA katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo, huku akibainisha kuwa bidhaa nyingi zinazouzwa kwenye maonesho hayo zimesafirishwa kupitia huduma za usafiri wa umma.

Akizungumzia usafiri wa reli, CPA Suluo amesema kuwa LATRA hushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kukagua na kuthibitisha ubora wa mabehewa, vichwa vya treni na miundombinu kabla ya kuanza kutumika.
“Tunapokagua vifaa hivyo nje ya nchi na kuvikubali, tunajua Watanzania watapata huduma salama,” amesema.
Kwa upande wa mabasi, amesema LATRA hupanga nauli za daraja la kawaida na la kati ili kuhakikisha wananchi wanamudu gharama, huku wakiwaachia wenye mabasi ya luxury kupanga nauli wenyewe ili kuongeza ushindani.
Kuhusu usafiri wa waya, Suluo amesema ni sekta mpya itakayovutia watalii, ikiwa sehemu ya juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kukuza utalii kupitia Royal Tour.
Amebainisha kuwa kanuni za kuendesha huduma hiyo zipo katika hatua za mwisho za kuidhinishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kuanza kutoa leseni.