Mgombea wa kiliberali nchini Korea Kusini, Lee Jae-myung, ameshinda uchaguzi wa urais nchini humo dhidi ya mpinzani wake wa kihafidhina Kim Moon Soo.

Mgombea wa kiliberali nchini Korea Kusini,  Lee Jae – myung ameshinda uchaguzi wa urais nchini humo dhidi ya mpinzani wake wa kihafidhina Kim Moon Soo na ambaye shirika la habari la nchini humo, Yonhap limeripoti kwamba amekubali kushindwa katika uchaguzi huo.

Kulingana na Yonhap, Lee ameshinda kwa asilimia 49.4 ya kura, wakati Kim akipata asilimia 41.1 huku idadi ya wapiga kura ikitajwa kuwa ilikuwa karibu asilimia 80.

Baada ya tume ya Kitaifa ya Uchaguzi kuthibitisha matokeo hayo, Lee, ataingia ofisini mara moja kuchukua nafasi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Yoon Suk Yeol, ambaye aliondolewa madarakani kwa kuiweka nchi hiyo katika sheria ya kijeshi mwishoni mwa 2024.

Kura za Wakorea Kusini zimebadili mwelekeo wa siasa nchini humo kwa kuiadhibu vikali serikali iliyopita, na sasa Lee anayetokea katika kambi ya upinzani inayoegemea mrengo wa kushoto atashika dola.