Bajeti Kuu Kuwasilishwa Bungeni leo
Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,DODOMA
Serikali inatarajia kuwasilisha Bajeti Kuu leo pamoja na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2025, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka ujao utagharimiwa kwa fedha za ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema bajeti hiyo ni ya mwisho katika Awamu ya Sita ya uongozi wa Serikali na ina umuhimu wa kipekee kwa sababu inaweka msingi wa kuelekea uchaguzi mkuu.
“Bajeti hii ni ya kihistoria. Kwa mara ya kwanza uchaguzi mkuu utahudumiwa kwa fedha za ndani. Wananchi wanapaswa kufuatilia kwa karibu kuona namna Serikali imepiga hatua kubwa za kimaendeleo,” alisema Msigwa.
Kuhusu Gawio la Serikali Msigwa amesema Serikali imepokea gawio la Shilingi trilioni 1.28 kutoka kwa mashirika ya umma kwa mwaka huu, hatua aliyosema ni rekodi mpya katika historia ya taifa.
Amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika mashirika ya umma, ambapo hadi sasa kiasi cha Shilingi trilioni 86 kimewekezwa.
“Kutokana na msingi huu wa uwekezaji imara, tunategemea gawio kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka,” alisema.
Aidha, amebainisha kuwa mafanikio haya pia ni matokeo ya utekelezaji wa falsafa ya R4 iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo inalenga kuongeza ufanisi, uwazi, uwajibikaji na tija katika taasisi za umma.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali, Msigwa amesema Awamu ya Pili ya mradi huo imefikia asilimia 90, huku gharama za utekelezaji wake zikiwa ni Shilingi bilioni 738.9.
Ujenzi huo unahusisha jumla ya majengo 34, ambapo sita kati yake tayari yamekamilika na kuanza kutumika na wizara husika. Miundombinu ya barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 59.1 inaendelea kujengwa, sambamba na mfumo wa umeme wa ardhini wenye urefu wa kilometa 42 ambao umefikia asilimia 59 ya utekelezaji.
Pia, ufungaji wa kamera za ulinzi umefikia asilimia 55, na kampeni ya upandaji miti inayoendelea tayari imewezesha kupandwa kwa miti 233,000 katika maeneo ya wazi na kandokando ya barabara ndani ya Mji wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Msigwa ametoa onyo kali kwa vijana, hususan wanafunzi wa vyuo vikuu, dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa kuandika taarifa za uchochezi au zinazolenga kuigombanisha serikali na wananchi wake.
“Nitumie nafasi hii kuwaonya vijana wetu wa vyuo vikuu kuacha kuichafua Serikali kupitia mitandao ya kijamii. Watumie mitandao hiyo kwa ajili ya kujielimisha, kufanya biashara au kujitangaza kwa njia chanya,” alisema.
Amesisitiza kuwa sheria ipo wazi na vyombo vya dola viko macho kwa ajili ya kuhakikisha matumizi ya mitandao yanazingatia maadili na sheria za nchi. “Kutokujua siyo sababu ya kuvunja sheria,” alionya.
