Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema wananchi wana kila sababu ya kudai haki na kuleta mabadiliko kupitia chama hicho ambacho kimekuwa mstari wa mbele kutetea usawa kwa wote.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Kiburugwa, Jijini Dar es salaam Profesa Lipumba amesema mwaka huu Watanzania wana bahati kubwa kwa kuwa CUF imesimamisha wagombea wa nafasi zote kuu — urais, ubunge na udiwani — ambao ni “watu wa watu” wazalengo na wana uchungu wa kweli kwa wananchi.
“Umaskini unaoendelea nchini ni matokeo ya sera mbovu za chama tawala, CCM. Tuliahidiwa vita dhidi ya maadui watatu — ujinga, maradhi na umaskini — lakini hadi sasa hawajaonyesha wamefikia wapi. Badala yake wanaendelea kutuambia watafanya nini kwa siku 100,” alisema Prof. Lipumba.

Ameongeza kuwa Tanzania imebarikiwa ardhi yenye rutuba ambayo inaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana endapo serikali itakuwa na sera makini za kilimo na viwanda. “Ni wakati wa kuwachagua viongozi watakaotumia fursa tulizonazo kujenga uchumi imara na kupunguza umasikini,” amesisitiza.
Aidha Prof. Lipumba amesema vyanzo vya kodi katika halmashauri ni vingi, lakini kutokana na ubadhirifu na miundombinu mibovu, huduma za afya, maji na elimu zimeendelea kuwa duni. Alitoa wito kwa wananchi wa Kiburugwa na maeneo mengine ya Dar es Salaam kuchagua viongozi waadilifu watakaowezesha maendeleo ya kweli.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi, Prof. Lipumba ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CUF, akisema hatua hiyo ndiyo njia pekee ya kuleta haki na mabadiliko ya kweli.
Prof. Lipumba pia amewataka Jeshi la Polisi kuhakikisha haki inasimamiwa wakati wa kampeni na uchaguzi, huku akionya dhidi ya vitendo vya kuchana mabango ya wagombea.
“Usitumie umaskini wa watu kuwapa pesa wachane mabango. Huko juu CCM wakanyeni watu wenu. Hatutaki vurugu, tunataka amani na hoja,” amesisitiza.
Amewataka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha mawakala wanakuwepo vituoni kabla ya kuanza kwa uchaguzi na kumtaka Naibu Katibu wa Tume, Kailima, kuhakikisha watendaji wote wanazingatia taratibu.
