Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea.
Waziri wa Afya Jenista Mhagama ameitaka Jamii na wadau hapa nchini kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya homa ya Ini ili kuweza kuutokomeza ugonjwa huo kama ilivyo dhamira ya Serikali.
Akizungumza katika Maadhimisho siku ya homa ya Ini Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Songea club uliopo Manispaa ya Songea, Waziri Jenista alisema kuwa jamii inapaswa kuchukuwa tahadhari ya ugonjwa huo ambao unaambukiza kwa njia ya kujamiiana au ikiwa mgonjwa mwenye jeraha atagusana na mtu mwingine.
Amesisitiza swala la kupima virusi vya homa ya ini ili kujuwa kama umeambukizwa au haujaambukizwa ni muhimu na si vinginevyo.

Waziri Mhagama alisema Serikali imeshusha matibabu ya homa ya ini mpaka ngazi ya zahanati na hivyo ametoa wito kwa Jamii kupima virusi vya ugonjwa huo kwa kuwa matibu yake yanatolewa bure na Serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed alisema Mkoa wa Ruvuma si kisiwa hivyo nao huko bega kwa bega na Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya homa ya ini.
” Tafiti za Kitaifa zilizofanywa kwa mwaka 2022/2023 zinaonesha kiwango cha maambukizi katika Mkoa wa Ruvuma kwa watu wenye umri wa miaka 15 ni asilimia 2.0 sawa na watu wawili katika Kila watu100″ alisema mkuu huyo wa Mkoa .
Baadhi ya wananchi wameipongeza serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuboresha miundombinu ya Majengo pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba jambo ambalo limekuwa likiwarahisishia kupata huduma za kiafya kwa ukaribu ikiwemo chanjo ya ini kwa watoto wadogo kuanzia 0 hadi miaka 5.

