Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAADHIMISHO ya kitaifa ya Siku ya Haki za Mtumiaji Duniani kwa mwaka 2026 yanatarajiwa kufanyika jijini Tanga Machi 15, yakilenga kuhamasisha ulinzi wa haki, usalama na ustawi wa watumiaji wa bidhaa na huduma nchini.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Machi 10, 2026, Mwenyekiti wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF), Daudi Goodluck Daudi, amesema maadhimisho hayo yatawapa wananchi fursa ya kupata elimu kuhusu haki na wajibu wao kama watumiaji wa huduma mbalimbali zinazodhibitiwa.

Amesema Jukwaa la Watumiaji Tanzania linaundwa na Mabaraza ya Ushauri ya Watumiaji kutoka mamlaka mbalimbali za udhibiti nchini ikiwemo EWURA CCC, LATRA CCC, TCAA CCC na TCRA CCC, ambayo hushirikiana kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma hizo.

Kwa mujibu wa Daudi, maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Bidhaa Salama, Watumiaji Wenye Kujiamini’, inayolenga kuhimiza upatikanaji wa bidhaa na huduma salama zinazokidhi viwango vya ubora ili kuwajengea watumiaji uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.

Amefafanua kuwa watumiaji wenye kujiamini ni wale wanaopata bidhaa na huduma salama, wanaofahamu haki na wajibu wao pamoja na kuwa na uwezo wa kuhoji ubora wa huduma wanazotumia.

Daudi amesema katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, TCF imeandaa shughuli mbalimbali za utoaji elimu kwa umma zitakazoanza Machi 10 hadi 26, 2026 kupitia vipindi vya vyombo vya habari pamoja na semina kwa makundi mbalimbali ya watumiaji.

Ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataweka msisitizo katika usalama wa huduma na bidhaa katika sekta mbalimbali zinazodhibitiwa, ikiwemo huduma za nishati na maji, usafiri wa anga, usafiri wa nchi kavu pamoja na huduma za mawasiliano.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA-CCC), Innocent Kyara, amesema baraza hilo linaipongeza Shirika la Ndege la Air Tanzania kwa kutekeleza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi baada ya kufanikisha kuwarejesha nchini Watanzania waliokuwa wamekwama Dubai.

Amesema kama Baraza la Watumiaji wa huduma za usafiri wa anga wanatoa pongezi kwa Air Tanzania kwa kuchukua jukumu lake la msingi la kuhakikisha Watanzania wanaendelea kutumia huduma za usafiri wa anga kwa usalama.

Aidha, ametoa rai kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga kuhakikisha wanakusanya taarifa muhimu kabla ya kupanga safari zao ili kufahamu mazingira na hali ya safari wanayoikusudia, hatua ambayo alisema huwasaidia kupanga safari kwa ufanisi zaidi.

“Wakati mwingine changamoto zinaweza kujitokeza licha ya mipango mizuri ya safari, lakini ipo mikataba ya kimataifa inayosimamia masuala ya usafiri wa anga ambayo inaelekeza wajibu wa nchi husika kuwahudumia abiria wanaokwama katika viwanja vya ndege,” amefafanua.

Kwa upande wake, Lugiko Lugiko aliyemwakilisha Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), amesema Siku ya Mtumiaji Duniani ni siku muhimu inayoadhimishwa kimataifa kwa lengo la kuhamasisha ulinzi wa haki za watumiaji.

Amesema kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza umuhimu wa upatikanaji wa bidhaa na huduma salama ili kuwajengea watumiaji ujasiri na imani katika huduma wanazozitumia.

“Kuna miongozo ya Umoja wa Mataifa inayozungumzia masuala ya ulinzi wa haki za mtumiaji na kaulimbiu hii inatokana na miongozo inayosisitiza namna haki za watumiaji zinavyopaswa kulindwa,” amesema Lugiko.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yanatoa ujumbe kwa pande zote mbili, watumiaji na watoa huduma, ambapo watumiaji wanahimizwa kudai huduma zilizo salama huku watoa huduma wakikumbushwa wajibu wao wa kutoa huduma zenye ubora na usalama.