Maandalizi ya uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo mkoani Mtwara yanaendelea vizuri ambapo hadi kufikia Februari 03, 2026 yamefikia zaidi ya asilimia 90.
Hayo yameelezwa na Mhandisi Felista Ndabita kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), wakati wa ziara ya kikazi iliyofanywa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa, Mha. Felista alieleza kuwa kwa sasa mtambo utakaotumika katika uchimbaji wa gesi asilia umeshasimikwa tayari kuanza uchimbaji wa visima hivyo.
“Kama mnavyoona, kazi ya ufungaji wa mtambo wa kuchimba umekaribia kabisa kukamilika; na vifaa na miundombinu wezeshi ipo katika hatua za mwisho za kukamilika. Matarajio ni kuanza uchimbaji wa visima Februari 09, 2026.” Alieleza Ndabita.
Kwa upande wake, Mjiolojia kutoka PURA Bw. Ebeneza Mollel alieleza kuwa PURA kama Mamlaka imeridhishwa na hatua iliyofikiwa na itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kuwa malengo ya kuongeza uzalishaji kutoka katika Kitalu hicho yanafikiwa.
Kwa sasa, Kitalu cha Mnazi Bay kina jumla ya visima vitano (5) vinavyozalisha gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 90 hadi 100 kwa siku.
Ongezeko la uzalishaji wa gesi asilia unaotarajiwa kufuatia uchimbaji wa visima hivyo utawezesha upatikanaji wa gesi zaidi kwa matumizi mbalimbali yakiwemo kuzalisha umeme, matumizi ya viwandani, majumbani na kwenye magari.









