Machifu kutoka maeneo mbalimbali nchini wamewasilisha maombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, wakimtambua kama Chifu Hangaya, wakiomba kuwa mlezi wa Tamasha la Machifu na kulifanya liendelee kufanyika chini ya ofisi yake.

Aidha, wamemuomba kufadhili tamasha hilo na kujenga uwanja wa Kisesa, wakipendekeza upewe jina la Chifu Hangaya kama sehemu ya kumuenzi.

Wakiwa katika Tamasha la Utamaduni la Bulabo la Kanda ya Ziwa 2025 lililofanyika Kisesa, wilayani Magu mkoani Mwanza, Rais Samia akiwa mgeni rasmi, viongozi hao wa jadi walimsifu kwa kuwa kiongozi mwelewa, muadilifu, anayeheshimu mila na amani, na mwenye upendo kwa watu wote bila ubaguzi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Chifu Antonia Tonisizya alisema kwa umoja wao wanamuunga mkono Rais Samia, kumtetea na kuhakikisha anakuwa salama wakati wote wa uongozi wake.

Katibu wa Kamati ya Maandalizi, Chifu Aron Mkomangwa aliwasilisha maombi hayo rasmi kwa Rais na kueleza kuwa tamasha hilo linatoa jukwaa kwa machifu kujadili masuala ya utamaduni, mila, urithi wa Afrika, pamoja na changamoto kama uhifadhi wa nyara na mazingira.

Kaulimbiu ya tamasha hilo ni kuhamasisha ushiriki wa uchaguzi mkuu na matumizi ya nishati safi.

Mtemi Kisendi Nkingwa wa pili, Mwenyekiti wa Watemi wa Wasukuma, alimkabidhi Rais Samia kiti cha kichifu cha miaka mitano kilichotengenezwa kwa mti wa mkola, chenye baraka zote za kichifu.