Kujengwa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Megawati 90, kuhudumia Chunya, Songwe

Atoa Wito REA kuweka kipaumbele maeneo yenye shughuli za Madini

Agusia ujio wa Kampuni ya Kuchimba Madini Chunya ya Anglo De Beers

Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Chunya

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Alhaji Batenga, ameweka wazi Mikakati Kabambe ya kuimarisha shughuli za uchimbaji madini Wilayani humo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Umeme (Substation) chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 90 hatua inayolenga kupunguza changamoto za upatikanaji wa nishati hiyo kwenye shughuli za madini na nyingine.

Katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary Oktoba 09 2025, Mhe. Batenga alisema kituo hicho kitajengwa katika eneo la Makongorosi – Chunya hivyo kitahudumia maeneo ya Chunya na Mkoa wa Songwe, huku akitolea mfano wa Mgodi mpya wa Shanta- New Luika, Mtambo wa uchenjuaji wa Anglo De Beers ambao upo mpakani mwa Chunya na Songwe na mgodi mpya wa Porcupine North katika eneo lililoongezwa baada ya upanuzi, upo Chunya.

Alisema hivi sasa wilaya hiyo inatumia megawati 9 pekee huku mahitaji halisi yakiwa si chini ya megawati 90, na kueleza, ‘’kupitia kituo hiki, tutaanza kuzalisha megawati 45 – lengo ni kufanikisha uchimbaji wa kisasa kwa gharama nafuu, na hivyo kuchochea uwekezaji zaidi. Wachimbaji wetu wanahitaji sana umeme na hapa ninapokea maombi mengi sana ya kufikishiwa nishati hiyo kwenye maeneo yao, na katika hili, nitalisimamia,” alisisitiza Batenga.

Kutokana na mahitaji hayo makubwa ya umeme hususan kwenye shughuli za uchimbaji, alitoa wito kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa kipaumbele cha kusambaza umeme kwenye maeneo yenye shughuli za madini wakati wakipeleka maeneo mengine kutokana na mahitaji makubwa jambo litakalosaidia kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kuongeza uzalishaji na kueleza kwamba.

Upatikanaji wa nishati hiyo utasaidia kuvutia uwekezaji zaidi kutokana na wilaya hiyo kubarikiwa utajiri wa rasilimali madini na kugusia ujio wa kampuni ya uchimbaji madini ya Anglo De Beers ambayo ina baadhi ya leseni zake Chunya huku tayari ikiwa imeanza uchimbaji Songwe eneo la Mbangala.

Vilevile, alitoa shukrani kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka kuipa kipaumbele sekta ya madini na hususan wachimbaji wadogo, na kueleza kwamba, zaidi ya leseni 1,500 zilitolewa kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa wilaya hiyo na kutoa ombi la kuendelea kutoa leseni zisizoendelezwa ili wale wenye nia ya kuziendeleza wachimbe.

Katika hatua nyingine, aliiomba Wizara ya Madini kufanya tafiti zaidi ili kugundua maeneo mapya yenye madini ili kuwawezesha wachimbaji kuchimba pasipo kubahatisha na kupongeza kwa kutolewa mitambo ya uchorongaji miamba. Kutokana na shughuli za uchorongaji kutokuwa nafuu, alishauri kupatikana mitambo yenye gharama nafuu zaidi ili kuwezesha wachimbaji wadogo kumudu gharama za utafiti, na kusema, ‘’ lakini sisi hatuchimbi tu dhahabu, hivi sasa kuna kiwanda cha kuchenjua shaba hivyo ninawaasa wachimbaji waanze kuangalia na madini hayo,’’ alisema.

Katika mazungumzo yake, akayataja maajabu ya kipekee ya tarafa mbili zinazounda wilaya hiyo za Kiwanja na Kipambawe, Batenga alisema, “kila moja ni ya kipekee, tarafa ya Kiwanja ni maalum kwa shughuli za madini na Kipambawe mahususi kwa kilimo cha tumbaku. Madini hayapo kabisa Kipambawe na hakuna uchimbaji huko na tumbaku haistawi kabisa eneo la Kiwanja huko kuna kilimo kwa kiasi kidogo tu kwa mazao ya chakula,’’ alieleza.

Akizungumzia mchango wa sekta hizo wilayani humo, alisema hivi sasa Wilaya ya Chunya inachangia asilimia 60 ya fedha za maendeleo kwenye mfuko Mkuu wa Serikali, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka asilimia 40 kwa miaka ya nyuma. “Tunatarajia kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, Chunya itachangia hadi asilimia 80, kutokana na mapato ya madini na tumbaku, na kuongeza kuwa hivi sasa Halmashauri, inanufaika kwa kupata kiasi cha shilingi bilioni 5, kutokana na mapato ya sekta hizo mbili kuu, madini na tumbaku.

#Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri