Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Madiwani wa Kamati ya Mipango, Miji na Mazingira na Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii ,Manispaa ya Kibaha wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata nne .
Kuridhishwa huko kumejidhihirisha wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi hiyo, iliyoongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, ambapo madiwani hao walitembelea na kukagua Mradi wa Dampo la Misugusugu, Ofisi za Taasisi zilizopimwa na kupewa hati, Zahanati ya Misugusugu, Ofisi ya Kata ya Visiga pamoja na Shule ya Msingi Maili 35.

Aidha, kamati hizo zimekagua miradi ya ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu pamoja na Shule ya Awali na Msingi Mwambisi katika Kata ya Kongowe.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo,Meya Dkt. Nicas, alisema kamati hizo zimeridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi waliyoikagua, huku akipongeza juhudi za Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa na timu ya wataalamu kwa usimamizi wa miradi.
“Tumejionea kazi nzuri iliyosimamiwa kwa weledi mkubwa, hakika Manispaa imepiga hatua kubwa ya maendeleo, ikiwemo kupima maeneo ya Taasisi na kuyapatia hati, jambo linaloimarisha usalama wa mali za umma na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma kwa wananchi,” alielezea Dkt. Nicas.
Vilevile alieleza, Manispaa hiyo itaendelea kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa viwango vinavyokubalika na kuwanufaisha wananchi .



