Na Mwanishi Wetu, JamhuriMedia, Geita

Ajali ya moto imeteketeza maduka na vibanda 17 vya biashara katika soko la Buseresere wilayani Chato Mkoa wa Geita hali iliyosababisha uharibifu na hasara kubwa ya mali.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita, Hamis Dawa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa vibanda na maduka yaliyoteketea yalikuwa na stoo za kuhifadhia bidhaa ambapo asilimia kubwa ya maduka yalikuwa tayari yamefungwa na kufanya kazi ya uokoaji kuwa gumu.

Amesema kazi ya kuzima moto na uokoaji ilichukua saa sita hadi usiku wa kuamkia kuamkia Juni 11, 2025 kutokana na msongamano mkubwa wa vibanda.

“Taarifa ilichelewa kufika kwetu kama Jeshi la Zimamoto, nawasihi sana wananchi watoe taarifa mapema, kwa sababu kutoka Geita mjini hadi Buseresere ni umbali wa kilomita 40.”

“Kabla ya zZmamoto kuwasili juhudi za wananchi ziliendelea, na kwa sababu vyumba vingi vilikuwa vimefungwa kulikuwa na ugumu kwenye kufanya suala la uokoaji,”amesema Kamanda Dawa.

Kamanda Dawa amesema chanzo cha moto bado hakijafahamika, lakini askari wanaendelea na uchunguzi kubaini kiini cha tukio kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa eneo hilo.

Amesema miongoni mwa maduka yaliyoathirika ni maduka ya jumla na rejareja ambapo kutokana na ukubwa wa ajali ya moto iliwalazimu kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).

Mwenyekiti wa kitongoji cha Buseresere, Kasezero Athuman amesema taarifa za awali ambazo hazijathibitishwa ni kuwa moto umetokana na watu waliokuwa wanafanya uchomeleaji wa vyuma.

Kasezero ameiomba serikali kuweka ofisi za zimamoto na uokoaji katika miji midogo ya Katoro na Buseresere kutokana na mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara kwenye maeneo hayo.

Mfanyabiashara katika soko la Buseresere, Alice Wanjala amesema katika ajali hiyo amepoteza mtaji wake wa sh milioni 30 ikiwemo mkopo kutoka Benki ya CRDB aliokuwa anarejesha sh milioni 1.4 kila mwezi.