Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Masijala ndogo imetupa maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ya kupinga mashahidi kufichwa katika kesi inayomkabili ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.

Pia, mahakama hiyo imeelekeza mshitakiwa asizuiwe kuzungumza na wakili wake au kupewa nyaraka bila ya kuwepo na sababu ya msingi.

Jaji wa mahakama hiyo, Elizabeth Mkwizu alitoa uamuzi huo na kusomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Livin Lyakinana kwa kuwa jaji huyo hakuwepo na alimpatia maagizo asome uamuzi wake kama alivyouandika.

Katika uamuzi huo leo Agosti 13, 2025, jaji Mkwizu alikataa maombi ya Lissu akisema hayana mashiko kisheria kwa sababu viapo vilivyopo mahakamani vinajitosheleza hivyo si lazima viwepo viapo vya waliotishiwa kutoa ushahidi dhidi ya Lissu kama ilivyoelezwa katika maombi kwenye kikao kilichopita.

Jaji Mkwizu alisema kiapo cha Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele kina taarifa za kweli kwa kuwa yeye ni ofisa wa serikali na taarifa zake ni rasmi na ndiye mwenye mamlaka ya kupeleleza na kupata taarifa.

Pia, alisema kwa sababu Mafwele ndiye anayepeleleza na ana uwezo wa kupata hizo taarifa na kuhusu taarifa za mashahidi hao kuwepo kwenye kiapo chake kama zingekuwepo zingeweza kuathiri ushahidi wenyewe.

Kuhusiana na suala la Lissu kutokupewa haki ya kusikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, Jaji Mkwizu alisema hakimu huyo alizingatia haki ya Lissu ya kusikilizwa kwa sababu mahakama bado ina fursa ya kuangalia muonekano wa shahidi akiwa katika kizimba cha mahakama.

Akitoa uamuzi wa maombi ya mshitakiwa kutokutaka kuguswa na askari magereza akiwa mahakamani wala nyaraka zake, Jaji Mkwizu alisema usiri wa mawasiliano kati ya mshitakiwa na wakili ni jambo la msingi lakini usiri huo una mipaka yake.

“Mawasiliano ya siri yanatakiwa kutunzwa, lakini yawe ukomo wake ili isiathiri haki hiyo ya usalama wa gereza na wafungwa, kwa hiyo mshitakiwa asizuiwe kuwasiliana na mawakili, kupewa nyaraka bila sababu za msingi. Magereza wana haki ya kumlinda mshitakiwa ndani na nje ya mahakama kwa usalama wake,” alisema Jaji Mkwizu.

Awali, mawakili wanaomuwakilisha Lissu mahakamani hapo walipinga uamuzi huo wakidai hapakuwa na sababu za msingi zilizotolewa kwa madai kuwa mashahidi hao waliodai kutishiwa hakuna viapo vyao walivyoviwasilisha mahakamani kama ushahidi wa madai hayo.

Wakili wa mpeleka maombi, Dk Rugemeleza Nshala alidai viapo vya hao mashahidi waliodai kwamba walitishiwa, vilipaswa viwepo ili hakimu atoe uamuzi wa haki lakini hilo halikufanyika.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa serikali, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliiomba mahakama itupilie mbali maombi ya Lissu na wakaomba mahakama ijiridhishe na kile kilichowasilishwa na waleta maombi.

‎Katuga alidai uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ambao unalalamikiwa ulitolewa kwa mujibu wa sheria na kwamba mahakama ilijikita katika ushahidi wa viapo viwili vilivyotolewa na Wakili wa Serikali, Mafwele.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na mashitaka matatu akidaiwa kutuhumu askari polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.