Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu leo imefanya uchaguzi wa viongozi wake wakuu kwa mafanikio makubwa, ambapo Jaji Modibo Sacko kutoka nchini Mali amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Mahakama hiyo.

Aidha nafasi ya Makamu wa Rais sasa itashikiliwa na Jaji Bensaoula Chafika kutoka Algeria.

Uchaguzi huo umefanyika wakati ambao Jaji Imani Daud Aboud kutoka Tanzania anamaliza rasmi kipindi chake cha pili cha uongozi kama Rais wa Mahakama hiyo.

Akihitimisha utumishi wake, Jaji Aboud alieleza kuhusu mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazoikabili Mahakama hiyo, hasa kutotekelezwa kwa maamuzi yake na baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

“Uchaguzi umeenda vizuri, najivunia urithi ninaouacha,” alisema Jaji Aboud, Rais mpya alikuwa Makamu wangu kwa kipindi hiki cha mwisho, tumefanya kazi kubwa pamoja kama viongozi na tumeibadilisha Mahakama hii kwa kiwango kikubwa.”

Akiangazia mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake Jaji Aboud alieleza kuwa Mahakama hiyo imepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa serikali mbalimbali na kufahamika si tu barani Afrika bali pia kimataifa. Aidha, alitaja mafanikio kama kufanikisha ujenzi wa jengo la kudumu la Mahakama hiyo ambalo limekuwa katika mipango kwa zaidi ya miaka 20 na sasa liko tayari kuzinduliwa ndani ya miezi michache ijayo.

Pamoja na mafanikio hayo alikiri kuwa changamoto kubwa inayoikabili Mahakama hiyo ni utekelezaji wa maamuzi yake. Alifafanua kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya moja kwa moja ya kuhakikisha utekelezaji wa hukumu zake jambo ambalo linahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa vyombo vingine vya Umoja wa Afrika, hasa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje.

“Hii si changamoto ya Mahakama yetu pekee, bali ni changamoto ya Mahakama nyingi za Afrika na hata za kimataifa,” alieleza Jaji Aboud.

“Tunaendelea na mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Afrika ili kuboresha utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama hii kwa manufaa ya wananchi wa Afrika.”

Amehimiza nchi wanachama kuhakikisha kuwa maamuzi ya Mahakama hiyo yanatekelezwa kwa kuwa Mahakama hii haikuanzishwa kwa jina tu, bali kwa lengo la kulinda na kutetea haki za binadamu barani Afrika.

Kwa upande wake Rais mpya Jaji Modibo Sacko ameahidi kuendeleza mikakati iliyoanzishwa pamoja na mtangulizi wake.

“Kama Makamu wa Rais nimeshiriki katika kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali, sasa nitaendelea kuhakikisha inakamilika kikamilifu ikiwemo utekelezaji wa maamuzi yatakayotolewa.”

Kwa sasa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu inatarajia kuendeleza juhudi za kuelimisha wananchi wa Afrika kuhusu uwepo wake na umuhimu wake katika kuhakikisha serikali zinawajibika kwa masuala ya haki za binadamu.

Uongozi huu mpya unatarajiwa kuleta msukumo mpya katika safari ya Mahakama hii kuelekea kuhakikisha haki, usawa na uwajibikaji barani Afrika.