Mahakama ya shirikisho nchini Marekani imesitisha ushuru mkubwa uliowekwa na Rais Donald Trump hatua ambayo ni pigo kubwa kwa sehemu muhimu ya sera zake za kiuchumi.
Mahakama ya Kimataifa ya Biashara iliamua kwamba sheria ya dharura, ambayo Ikulu ya White House iliitisha, haimpi rais mamlaka ya upande mmoja ya kutoza ushuru kwa takriban nchi zote duniani.
Mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini Manhattan ilithibitisha kuwa Katiba ya Marekani inalipa baraza la Congress mamlaka ya kipekee ya kudhibiti biashara na nchi nyingine, na kwamba jukumu la rais la kulinda uchumi halichukui nafasi ya mamlaka hayo.
Mahakama pia ilisitisha ushuru tofauti ambao Trump aliziwekea China, Mexico, na Canada tangu arejee Ikulu ya White House, kujibu kile alichokitaja kuwa utitiri usiokubalika wa dawa za kulevya na wahamiaji haramu nchini Marekani.
