Na Mwandishi Wetu, JamhiriMedia, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu afikishwe mahakamani hapo Mei 19, 2025 na Mkuu wa Gereza la Ukonga.
Lissu anayekabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo alishindwa kufikishwa Mahakamani kutokana na hoja za upande wa Jamhuri kwamba kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya mtandao, huku Lissu naye akigomea kushiriki kesi hiyo kwa njia ya mtandao.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini ambaye ametupilia mbali hoja za upande wa Jamhuri uliotaka kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya mtandao kutokana na sababu mbalimbali.
Katika uamuzi wake leo, Hakimu Mhini amekubaliana na hoja za Jopo la Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mpale Mpoki ya kwamba shauri hilo lilipaswa kuendeshwa wakati Mshtakiwa akiwepo mahakamani kwani zipo baadhi ya nyaraka anazotakiwa kusaini kwa sababu alitakiwa kusomewa maelezo ya awali (Ph).
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala amesema “Kile kilichofanywa na mahakama kwamba kesi hii isikilizwe kwa njia ya mtandao ni sahihi kanuni zinaruhusu lakini akaendelea kusema kwamba Mahakama hii haina Mamlaka ya kuamuru Magereza namna ya kukaa na mshtakiwa gerezani,”.

Naye Wakili Peter Kibatala, ambaye ni miongoni mwa Mawakili wanaomtetea amesema maamuzi ya Mahakama kukubaliana na mapingamizi yao na kuagiza mteja wao aletwe mahakamani kusomewa maelezo ya awali ni ya kushujaa na yanayolinda heshima ya muhimili huo wa dola
Wakili Kibatala ametoa wito pia kwa wananchi watakaohudhuria shauri hilo siku za usoni kuwa watulivu na kuhakikisha wanafuata miongozo ya Mahakama, katika maamuzi ya mapingamizi hayo.