đź”¶Miradi ya kimkakati yaongeze matarajio ya maendeleo
Na Mwandishi Wetu, JamhutiMedia, Mahenge
MKOA wa Kimadini wa Mahenge umeanza kwa kasi katika ukusanyaji wa mapato ya madini kwa mwaka wa fedha 2025/2026, baada ya kukusanya shilingi milioni 270 ikiwa ni asilimia 62 ya lengo la shilingi milioni 433 la kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba, 2025. Lengo la mwaka lililowekwa ni shilingi bilioni 1.3.
Akizungumza na waandishi wa habari, hivi karibuni Afisa Madini Mkazi wa Mahenge (RMO), Jonas Mwano, alisema mafanikio hayo yametokana na ongezeko la uzalishaji wa madini ya vito pamoja na kuimarika kwa mifumo ya usimamizi na udhibiti wa rasilimali hizo.

Mwano alibainisha kuwa Mahenge, inayojumuisha wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi, imeendelea kuwa kitovu cha uzalishaji wa madini ya vito, madini ya viwandani kama graphite, pamoja na madini ya ujenzi ikiwamo kokoto, mchanga na mawe.
Alisema licha ya eneo hilo kutegemea zaidi uzalishaji wa madini ya vito, miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuanza utekelezaji itachochea kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.
“Miradi hiyo inajumuisha kampuni za Faru Graphite na Duma ambazo tayari zimepata leseni na zinajiandaa kuanza uzalishaji,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwano, miradi hiyo itachangia kuboresha miundombinu ya Mahenge ikiwamo upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya migodi na matumizi ya majumbani, pamoja na ujenzi wa barabara za lami.

“Barabara kutoka Ifakara hadi Ulanga imekuwa changamoto kwa muda mrefu. Ili makontena ya Kinywe yasafirishwe kwa usalama, lazima kuwe na barabara ya uhakika. Tuna matumaini uwekezaji huu utafungua ukurasa mpya,” alisisitiza.
Aidha, alisema kampuni hizo zinatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo, ambapo Faru Graphite itaanza kwa kuajiri watu 500, huku Duma ikitarajia kutoa ajira 300.
Kwa upande wao, wachimbaji wadogo wameiomba Serikali kuangalia namna ya kurahisisha upatikanaji wa madini katika masoko ya ndani.
Khalid Njechere, mnunuzi wa madini ya vito, alisema baadhi ya wawekezaji wakubwa wanauza madini nje ya nchi kwa kibali maalum, hali inayowaacha wachimbaji wadogo bila malighafi ya kutosha.

“Tunaomba Serikali ifanye mazungumzo na wawekezaji wakubwa ili angalau sehemu ya madini yao ibaki hapa nchini. Sokoni tunapata changamoto kubwa kupata madini,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Kampuni ya RGI, Shafii Daome, alisema kampuni hiyo inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya spinel imeajiri Watanzania 64 na wageni sita, huku ikiendelea kutekeleza miradi ya kijamii ikiwamo ujenzi wa ofisi za kata na uchongaji wa barabara ya kilomita saba ambayo imekuwa ikileta changamoto wakati wa mvua.
Daome alisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya machimbo.







