Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Taasisi zote za Serikali ambazo bado hazijajiunga na Mfumo wa Kielektroni wa Mawasiliano baina ya Mifumo ya Serikali (Government Enterprise Service Bus – GovESB), kuhakikisha zinafanya hivyo ifikapo Julai 30, 2025.
Majaliwa ametoa agizo hilo June 23,2025 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park.

Amesema, “Taasisi zote za umma ambazo hazijajiunga na mfumo huu, mwisho wa kufanya hivyo ni Julai 30 mwaka huu,wote mnatakiwa mmeshaingia kwenye GovESB huu ni msisitizo alioutoa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, kwamba pindi eGA watakapokamilisha maandalizi, kila Taasisi ipeleke mfumo wake,” amesema Waziri Mkuu.
Ameeleza kuwa hadi sasa idadi ya Taasisi zilizounganishwa ni chache licha ya kwamba mfumo huo hauna gharama ya kujiunga, wala huhitaji upangaji wa bajeti maalum.
Majaliwa amesisitiza kuwa matumizi ya GovESB ni hatua muhimu katika mageuzi ya utoaji wa huduma serikalini, kwani mfumo huo utawezesha taasisi kuwasiliana kwa haraka, ufanisi na kwa njia ya kidijitali, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

“Mfumo huu una faida kubwa katika utumishi wa umma kwani utaongeza ufanisi, uwazi, na kuondoa urasimu unaoweza kuchelewesha huduma kwa wananchi,” ameongeza.
GovESB ni jukwaa linaloratibiwa na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), likiwa na lengo la kurahisisha mawasiliano na uhamishaji wa taarifa kati ya mifumo mbalimbali ya taasisi za umma, kwa ajili ya kutoa huduma bora, za haraka na kwa gharama nafuu.


