*Asema Rais Samia anatosha, aomba wananchi kumchagua kwa kishindo
*Asema Salma Kikwete ana uwezo na dhamira ya kuwatumikia wananchi wake
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amezindua kampeni za Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Mchinga, Salma Kikwete, zilizofanyika Kijiji cha Rutamba mkoani Lindi.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana, amesema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/2030 imejielekeza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kote nchini ikiwamo Mchinga.
Katika kipindi kilichoisha Rais Samia Suluhu Hassan ameleta hapa miradi mikubwa, ya kati na midogo. Anafanya hivi kwa kutambua wananchi wanapaswa kuhudumia, hata ilani hii imeonyesha maeneo mengine yatakayotekelezwa mkoani Lindi,” amesema.

Majaliwa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, amesema wana Lindi wanapaswa kumchagua Rais Samia ili aendelee kutekeleza miradi ya gesi, bandari ya uvuvi Kilwa, ujenzi upya wa Barabara ya Dar es Salaam hadi Lindi, maboresho ya uwanja wa ndege wa Lindi, ujenzi wa reli ya kanda ya kusini pamoja na kuiunganisha Lindi kwenye Gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika.
Amesema Rais Samia ameleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na ilani hiyo imesheheni miradi inayokwenda kutekelezwa.
Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030 imeonyesha kuwa kutaanza kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Ngongo-Ngapa, Mandawa hadi Chikundi, barabara hii itakuwa ni mkombozi kwa wakazi wa maeneo haya na itafungua uchumi kwa wana-Lindi,” amesema.

Vilevile, amesema kwa miaka mitano iliyopita, Mchinga imefanikiwa kuwa na magari ya wagonjwa manne pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vilivyosaidia kuboresha huduma za afya jimboni humo.
Salma Kikwete amejikita katika kuwahudumia wananchi, kwa namna jimbo hili lilivyokaa linahitaji mtu mahiri na mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake, hakika Salma ameonyesha ameweza, mchagueni tena,” amesema.
Kwa upande wake, Salma, amesema katika kipindi chake amefanikiwa kushirikiana na wana Mchinga kutafuta majibu ya changamoto yaliyo katika jimbo hilo.
Tumepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na changamoto zetu, hali ilivyo leo si sawa na tulikotoka, tumepata mafaniko katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, nishati, elimu, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi, nikipata ridhaa tena tutafanya makubwa zaidi,” amesema.
Katika kipindi cha miaka mitano, amesema ametekeleza mradi wa maji kutoka Ngapa utakaovifikia vijiji vingi vya Mchinga.

Kama hiyo haitoshi tumefanikiwa kujenga zahanati, tutaongeza juhudi za ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema.
Naye Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amesema Rais Samia ameonyesha kuwa anatosha katika nafasi ya Urais, kwa sababu katika kipindi kifupi amefanya mambo mengi na tumpe nafasi aendelee.
Alipata Urais katika wakati ambao hakutarajia, lakini amefanya kazi nzuri, tutanufaika mara dufu, tukimpa nafasi, nimeangalia orodha ya mambo yaliyo kwenye ilani kwa hakika amejipanga,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wagombea ubunge wa Lindi, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, amesema wana-kusini watamchagua Rais Samia kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika mkoa huo ikiwamo utoaji wa ruzuku ya pembejeo kwenye mazao.



