*Ni kwa ajili ya uchorongaji na utafiti wa madini.
*Asema ni mwendelezo wa juhudi za Rais Dkt. Samia kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo.
*Atoa wito kwa wachimbaji wadogo kuuza madini ndani ya nchi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua mitambo kumi ya uchorongaji na vifaa vya utafiti wa madini yenye thamani wa shilingi bilioni 12.41 kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambayo itapunguza changamoto za wachimbaji wadogo ya kufanya uchimbaji bila kuwa na taarifa za kijiolojia.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo uliofanyika leo Jumanne (Juni 24, 2025) kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa juhudi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo wa madini na kuwawezesha kuongeza uzalishaji.

“Oktoba 2023 Rais Dkt. Samia, alizindua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Kutokana na wingi wa wachimbaji wadogo nchini na mwitikio chanya wa wachimbaji wadogo alielekeza Wizara ya Madini kuongeza mitambo mingine”
“Mitambo hiyo mitano imeshatoa huduma ya uchorongaji kwa wachimbaji 16 katika maeneo mbalimbali nchini na kuchoronga jumla ya mita 3,450.37”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kuongezeka kwa mitambo ya uchorongaji maalumu kwa wachimbaji wadogo kutaleta mageuzi na manufaa makubwa katika sekta madini. “Moja ya faida kubwa za mitambo hiyo, ni pamoja na kuongeza chachu ya ukuaji wa shughuli za wachimbaji wadogo nchini kwa kuwa itawawezesha upatikanaji wa taarifa za uhakika za jiolojia”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kuendelea kuuza madini katika viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu ili kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi nchini. “Na wale ambao wanashughulika na usafishaji wa madini, nendeni mkauze kwenye masoko yetu 43 yaliyopo na vile vituo 109, hakikisheni mzunguko wa madini unaanza kunufaisha Taifa letu badala ya kutorosha madini, kama kweli wewe ni mzalendo wa Taifa hili, popote utakapozalisha madini nenda kwenye masoko ya ndani ya nchi.”

Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha unaoishia, Sekta ya Madini imefanikiwa kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali kiasi cha shilingi trilioni 1.01. “Pamoja na maboresho haya, kwasasa katika benki Kuu ya Tanzania inahifadhi ya tani 5.7 na kuifanya Tanzania kuwa ndani ya kumi bora ya nchi zenye hifadhi ya dhahabu Afrika”.
Aidha, ameongeza kuwa katika miaka miaka ya minne ya Rais Dkt. Samia madarakani, sekta ya madini imeshuhudiwa ikifanya mapinduzi makubwa ikiwemo kuongeza mchango wake katika pato la taifa ambapo mpaka sasa inachangia asilimia 10.1 kabla ya mwaka wa kimalengo kufika .

Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa uamuzi wake wa kuamua kuisimamia sekta ya madini ikiwemo kuwawezesha wachimbaji wadogo nchini.
“Madini ni sayansi na madini ni biashara, kwa maboresho haya, sasa watanzania wanachagamkia fursa katika sekta ya madini, wachimbaji sasa wanatosha kuchimba, wachimbaji wadogo tupo pamoja na Serikali yetu, hakika imetuheshimisha.”





