WAZIRI MKUU, na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa leo Julai 2, 2025 ametangaza rasmi kutokugombea tena ubunge wa jimbo la Ruangwa baada ya kulitumikia jimbo hilo kwa miaka 15.

Akizungumza na wajumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya ya Ruangwa Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote ambao amekuwa mbunge wa jimbo hilo.

“Imefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa Wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili Kauli mbiu yetu ya Ruangwa kwa maendeleo inawezekana iweze kusonga mbele zaidi.”

Aidha, ametoa wito wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote wenye nia ya kugombea ubunge wa jimbo hilo.

Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watia nia wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Ruangwa Julai 2, 2025, kwenye Ofisi ya CCM Wilaya Ruangwa. Kutoka kushoto ni Mhandisi Phillip Undile Makota, Katibu wa CCM Wilaya Ruangwa , Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi Hassan Jarufu, Mparuka Hashim Mtopela, Bakari Nampenya Kalembo, Fikiri Boniface Liganga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi Wana-Ruangwa kuendelea kushikamana na itakapofika siku ya uchaguzi waweze kuchagua wagombea wote watakaowakilisha chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi huo.

“viongozi wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dkt. Nchimbi watakapokuja tujitokeze kwa wingi kwenye mikutano tusikilize sera, lakini siku ya kupiga kura tuwapigie kura nyingi za kutosha.”

Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Viongozi wakuu wa chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuwatumikia wana Ruangwa.

Mheshimwa Majaliwa alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa mwaka 2010 na amehudumu kwa kipindi cha miaka 15.

aziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa, akiwapongeza baadhi ya watia nia wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Ruangwa Julai 2, 2025, kwenye Ofisi ya CCM Wilaya Ruangwa. Kutoka kushoto ni Mhandisi Phillip Undile Makota, Katibu wa CCM Wilaya Ruangwa , Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi Hassan Jarufu, Mparuka Hashim Mtopela, Bakari Nampenya Kalembo, Fikiri Boniface Liganga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa, akiwapungia mkono baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya kwenye Ofisi ya CCM Wilaya Ruangwa Julai 2, 2025.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)