Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Shirika la Viwango Tanzania kutokuwa na huruma na bidhaa zisizokuwa na ubora kwani Serikali inataka soko la Tanzania liwe na bidhaa bora, salama na zenye kuleta tija kwa mlaji na kwa uchumi.
Amewataka wazalishaji wa bidhaa na huduma, wahakikishe wanazingatia taratibu za vipimo, uthibitishaji wa ubora, na uboreshaji wa mifumo ya uzalishaji. “Muhakikishe bidhaa zenu zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa vilivyowekwa na TBS”.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Juni 4, 2025) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jingo la maabara na ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kufuatwa kwa viwango vya ubora.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafanyabiashara na waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, wana wajibu wa kuhakikisha bidhaa wanazoingiza nchini ni salama, zimeidhinishwa na zina alama ya ubora kutoka TBS au taasisi zinazotambulika.
“…Msikubali kubeba lawama ya kuruhusu bidhaa isiyokuwa na ubora halafu ikaua Watanzania, haifa haifai peleka kuiteketekeza na tunauhakika na maabara zetu. Tanzania sio shimo la bidhaa zisizokuwa na ubora.”
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua kuwa viwango vya ubora si tu vinahusiana na bidhaa bora, bali vinaimarisha afya na uchumi imara wa nchi. “Viwanda vyetu vinapaswa kuzalisha bidhaa ambazo zinaweza kununulika hata nje ya nchi, tunataka mataifa mengine yakimbilie bidhaa zetu.”

Amesema mradi huo unakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya afya kupitia usimamizi wa ubora wa bidhaa, vifaa tiba, vyakula, vipodozi na kemikali mbalimbali. “TBS ni mlinzi wa viwango; na kwa miundombinu hii mipya, huduma zitaimarika na kuchangia kulinda afya za wananchi.”
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na miongozo yake ya kuhakikisha Taifa linazidi kupata maendeleo.
Akizungumzia kuhusu viwango vya ubora wa bidhaa, Dkt. Jafo amesema Serikali inataka kuhakikisha viwango vinazingatiwa na wanataka nchi iendelee kuheshimika kwa upande wa viwango na maabara inayojengwa ni kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amesema lengo la kujenga jingo hilo ni pamoja na kusogeza huduma za viwango karibu na wananchi hasa wa Kanda ya Kati, kupunguza utegemezi wa maabara za Dar es Salaam na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa ubora wa bidhaa na huduma.
Dkt. Ashura amesema kuwa ujenzi huo ambao umefikia asilimia 76 unatarajiwa kukamilika Agost, 2025 na utagharimu shilingi bilioni 25.3. Kukamilika kwa ujenzi wa jingo hilo kutapunguza msongamano wa sampuli za bidhaa mbalimbali katika maabara za Dar es Salaam.
