Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ongezeko la majimbo mapya nane (8) ya uchaguzi kwa Tanzania Bara, na kufanya jumla ya majimbo ya uchaguzi kufikia 272, ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 2025.
Akizungumza katika Mkutano wa Kitaifa wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi na Vyama vya Siasa uliofanyika jijini Dodoma Leo Julai 27,2025 Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, amesema mabadiliko hayo ni sehemu ya maboresho ya mfumo wa uchaguzi ili kuendana na ongezeko la watu na mahitaji ya uwakilishi wa wananchi kwa usawa zaidi.

Aidha, amebainisha kuwa kata tano mpya zimeongezwa, na sasa Tanzania Bara ina jumla ya kata 3,960, hatua inayolenga kuboresha uwakilishi wa wananchi na kurahisisha usimamizi wa uchaguzi kwenye ngazi za msingi.
“Mabadiliko haya yamezingatia takwimu rasmi za idadi ya watu kutoka NBS, migawanyo ya kijiografia, na kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema kuwa kalenda ya uchaguzi imeshazinduliwa rasmi(Julai 26,2025)ambapo utoaji wa fomu kwa wagombea utafanyika kuanzia Agosti 9 hadi 27, 2025, huku kampeni zikiruhusiwa kuanza Agosti 28 hadi Oktoba 27.

Amesisitiza kuwa kila hatua ya maandalizi imekuwa ikitekelezwa kwa uwazi na kwa kushirikisha vyama vya siasa, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha uchaguzi wa haki na wa kuaminika.
Amekumbusha kuwa kampeni za uchaguzi ni fursa ya hoja, si matusi, na kwamba viongozi wote wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kuhamasisha uchaguzi wa amani na maridhiano
Kutokana na hatua hiyo Viongozi wa vyama vya siasa waliopata nafasi ya kuchangia katika mkutano huo, wamesema wanaridhishwa na maandalizi ya uchaguzi na wamepongeza tume kwa kuwapa nafasi ya kushiriki mchakato wa uchaguzi tangu hatua za amesema.

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF, amesema maandalizi ya mwaka huu yameonesha mwelekeo chanya zaidi ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.
“Kupata daftari la kudumu la wapiga kura kwa wakati kumeongeza ufanisi katika maandalizi yetu ya kampeni,tunaamini mazingira ya uchaguzi wa haki yanawezekana,” amesema.
Prof. Lipumba amezungumza kuwa kwa uchaguzi huu kila kitu kinaenda kwa uwazi utofauti wa chaguzi zilizopita na mwaka huu hali iliyotoa Uhuru kwa Chama chake kujipanga kwa kina kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu uchaguzi wa mwaka 2025.
” Tumeshakamilisha mapitio ya Ilani ya Uchaguzi, tumeanzisha mchakato wa kuwajengea uwezo wagombea wetu kupitia mafunzo ya maadili, mikakati ya kampeni, na mawasiliano ya kisiasa,tumeanzisha vikosi kazi vya kimkakati ngazi ya kitaifa hadi mkoa kwa ajili ya kusimamia maandalizi hayo kwa ukamilifu, “amesema na Ku ongeza;

Kwa kiwango fulani, tuna imani na jitihada zinazoendelea kufanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), hasa katika kuanzisha mchakato wa mashauriano na vyama vya siasa,hata hivyo, bado tunasisitiza umuhimu wa uwazi zaidi, ushirikishwaji mpana wa wadau na uhakiki wa daftari la wapiga kura ili kuhakikisha kila raia mwenye sifa anapata nafasi ya kushiriki, “ameeleza .
Amesema CUF imeweka mkazo mkubwa katika kuwaelimisha wagombea na wafuasi weke kuhusu umuhimu wa kutumia lugha ya staha, kushindana kwa hoja na kuheshimu kanuni za demokrasia.
“Kupitia mafunzo ya ndani ya chama, tunasisitiza kampeni za kistaarabu, za kuunganisha Watanzania badala ya kuwagawa,tumeunda pia kamati maalum ya maadili ya uchaguzi itakayoshughulikia nidhamu ya wagombea na wanachama wakati wote wa kampeni, ” amesema Prof.Lipumba.

Katika hatua nyingine,nao Viongozi wa vyama vya siasa wameeleza mikakati ya kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana, kwa kuwawezesha kugombea majimbo ya wazi, kutoa mafunzo ya uongozi, na kuwahamasisha kushiriki siasa za hoja.
Juma Ally Khatib, Mwenyekiti wa ADA-TADEA, amebainisha kuwa wanaendelea kuweka vipaumbele vya wazi vya ushiriki wa wanawake na vijana kupitia viti maalum, nafasi za uongozi ndani ya chama na kuandaa makongamano ya hamasa.
Aidha amesema wameweka mikakati ya kuhakikisha wanawake na vijana wanashiriki kama wagombea wa majimbo ya wazi kwa kuwapatia mafunzo, msaada wa rasilimali na kuondoa vikwazo vya kisiasa na kijamii vinavyowakwamisha.
“Tunaamini ushiriki wao ni muhimu katika kuimarisha demokrasia ya kweli,hatuchukulii wanawake na vijana kama mapambo, bali tunawatambua kama nguvu ya mabadiliko na maendeleo.”amesema.


