Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Mchakato wa kutangaza rasmi majina ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 unaoongozwa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, umeendelea kusogezwa mara kadhaa huku waandishi wa habari wakilazimika kukesha katika Ukumbi wa NEC Makao Makuu ya CCM, Dodoma.
Awali, kikao hicho kilipangwa kufanyika jana, Julai 28, 2025, saa 11 jioni, lakini kikasogezwa hadi usiku wa manane kwa madai ya kukamilisha taratibu za ndani za chama. Waandishi wa habari waliokuwa wamefika mapema kwa ajili ya kufuatilia matangazo hayo walilazimika kusubiri hadi saa 10 alfajiri bila mafanikio ya kupata majina.

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, waandishi walipewa taarifa kwamba tangazo hilo lingefanyika tena leo, Julai 29, saa 4 asubuhi, jambo lililowalazimu kurejea kwenye maeneo ya mkutano kwa matarajio mapya. Hata hivyo, muda huo ulipofika, kikao kilisogezwa tena na kuahirishwa hadi saa 6 mchana.
Taarifa kutoka ndani ya chama zinaeleza kuwa kucheleweshwa kwa matangazo hayo kunatokana na mchakato wa kuhakikisha majina ya wagombea yanapitishwa kwa umakini, ikiwa ni pamoja na kupitia mapendekezo ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM yaliyokamilika usiku wa kuamkia leo.
CPA Amos Makalla anatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari leo mchana mara baada ya vikao vya ndani kukamilika, na kuwatangaza wagombea wa Ubunge wa Majimbo, Viti Maalum vya Ubunge na Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar.

Hali ya kusubiri kwa muda mrefu imezua taharuki miongoni mwa waandishi wa habari na wadau wa siasa huku wengi wakitaka kujua hatma ya wagombea waliopitishwa na chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Pamoja na kucheleweshwa kwa hatua hiyo, viongozi wa CCM wameendelea kuwahakikishia wanachama na wananchi kwamba mchakato huo utazingatia misingi ya demokrasia ya chama na kuleta wagombea bora watakaoleta ushindi wa kishindo.
Wadau wa siasa na wananchi kwa ujumla wanatarajia kwa hamu kuona orodha ya mwisho ya wagombea, jambo litakalokuwa ishara rasmi ya CCM kuanza kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu.