Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mataifa kuhakikisha kunakuwa na hatua za pamoja, mshikamano wa kimataifa, na uwekezaji endelevu ili kuhakikisha uchumi endelevu wa bahari, kupunguza uchafuzi wa mazingira pamona na kulinda bioanuwai ya baharini.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari (UNOC3) akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo unaofanyika Jijini Nice nchini Ufaransa.
Amesema hapana budi kuwa na hatua za ujasiri zikazoratibiwa kwa ufanisi ili kuhakikisha maendeleo makubwa katika uendelevu wa bahari. Makamu wa Rais ameongeza kwamba ni muhimu kuongeza ufadhili katika kushughulikia changamoto za bahari, kwa kuzingatia zaidi kusaidia nchi za kipato cha chini na nchi zinazoendelea za Visiwa Vidogo, ambazo zinakabiliwa na ufinyu wa bajeti na mizigo ya madeni inayokwamisha kufikia ahadi zilizofanywa za utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu namba 14.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuhakikisha utekelezaji kamili wa Mkataba wa Bahari Kuu (BBNJ), kushughulikia tishio la uchimbaji madini wa bahari kuu usio endelevu pamoja na kuanzishwa kwa vyombo vya kisheria ili kukabiliana na uchafuzi wa plastiki. Pia amesema ni vema kuimarisha sera za kisayansi ili kukuza uhamishaji wa teknolojia, kutumia uwezo wa uvumbuzi, kuunganisha maarifa ya jadi na asilia na matumizi ya taarifa za wakati halisi ili kuwa na usimamizi bora wa bahari.
Aidha, Makamu wa Rais amesema ni lazima kuwa na ushirikiano jumuishi na wenye usawa unaowezesha jamii za watu wa pwani kuwa wahusika wakuu katika jukumu la kulinda na kuvumbua masuluhisho mbalimbali ya uendelevu wa bahari.
Vilevile Makamu wa Rais amesema Tanzania imechua hatua mbalimbali muhimu katika kuimarisha usimamizi wa bahari zikiwemo kuongeza maeneo ya hifadhi ya bahari katika maeneo ya maji kuhakikisha yanafikia lengo la asilimia 20 ifikapo mwaka 2030. Pia uwepo wa juhudi za uhifadhi na usimamizi shirikishi unaoongozwa na jamii unaohusisha ushirikishwaji wa wadau na wenyeji katika kufanya maamuzi, jambo linalopelekea kuongezeka kwa hali ya kuipenda na kuilinda bahari kwa wenyeji na hivyo kujenga uwezo wa ustahimilivu kwa jamii za pwani.

Ametaja hatua nyingine mbalimbali zilizochukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na kutunga na kusimamia sheria za kupambana na uvuvi haramu sambamba na kuimarisha mifumo ya uangalizi, udhibiti na ufuatiliaji. Halikadhalika kuandaa mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Buluu, ambao unaainisha mipango mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya baharini, kuvutia uwekezaji, kukuza utafiti na uvumbuzi na kuhakikisha uendelevu wa mazingira.
Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Mataifa mengine, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, na jumuiya za kiraia ili kujenga mustakabali wa bahari stahimilivu na yenye tija.
Mkutano huo unawakutanisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa, Asasi za Kiraia pamoja na Sekta binafsi kwa lengo la kuhamasisha utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu namba 14 (SDG 14) linalolenga kuhifadhi na kutumia kwa uendelevu rasilimali za bahari, bahari kuu na mazingira ya pwani.

Kauli mbiu ya Mkutano huo ambayo ni “Accelerating action and mobilizing all actors to conserve and sustainably use the ocean” inalenga kuhamasisha wahusika wote kuhifadhi na kutumia bahari kwa maendeleo endelevu.

