Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mheshimiwa Kanali Mstaafu Kembo Campbell Mohadi amewasili nchini Agosti 30. 2025 kwa ziara ya kazi ya siku mbili hadi Agosti 31 2025 kwa mwaliko wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango.
Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Makamu wa Rais Mohadi alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Akiwa nchini, Mheshimiwa Makamu Rais Mohadi atakuwa na mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango Ikulu jijini Dar es Salaam na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.
Aidha, Mheshimiwa Mohadi atatembelea Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha, Chuo cha Kilimo na Mifugo kilichopo Kaole, Bagamoyo na Kituo cha Urithi wa Ukombozi barani Afrika cha jijini Dar es Salaam.







