Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Licha ya Mkoa wa Pwani kuongoza kwa idadi ya viwanda nchini, unakabiliwa na changamoto ya baadhi ya viwanda kulipa kodi katika Mkoa wa Dar es Salaam badala ya Pwani, jambo linalodidimiza mapato ya mkoa.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa , Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, alieleza kuwa hali hiyo imekuwa ya kukatisha tamaa.
“Tunalalamikia changamoto hii kwa mwaka wa nne sasa, viwanda vingi vimejengwa Pwani lakini makao makuu yao yapo Dar es Salaam, Mfano, takribani viwanda 78 vinasomeka Dar es Salaam, na viwanda 95 hulipa kodi nje ya mkoa kwa upande wa serikali za mitaa, hali ambayo inakatisha tamaa ,” alisema Kunenge.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Kunenge alisisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi kuhusu viwanda vilivyopo pamoja na mapato yake, kwa lengo la kuongeza pato la Mkoa wa Pwani.
Aidha, aliwataka maofisa biashara katika mkoa huo kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa karibu ili kupata takwimu sahihi za viwanda vikubwa, vya kati na vidogo.
Kunenge pia alibainisha kuwa mkoa umejipanga kushirikiana na Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wazawa kuanzisha viwanda vidogo.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Dkt. Godwill Wanga, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona takwimu nyingi za viwanda vya Pwani zinatolewa na makampuni yenye makao makuu Dar es Salaam.
“Inashangaza kuona mkoa huu una viwanda vingi lakini unapata asilimia ndogo ya pato la taifa, Dar es Salaam ina asilimia 17 , wakati Pwani ina asilimia 2 pekee,” alisema Dkt. Wanga.

Aliongeza kuwa Pwani inazidiwa hata na mkoa kama Rukwa (2.1%), ambapo mikoa michache ambayo Pwani imeizidi ni Simiyu (1.8%), Songwe (1.8%), Katavi (1.3%), Njombe (1.8%), Singida (1.9%) na Lindi (1.9%), licha ya kuwa mikoa hiyo iko pembezoni lakini inatoa Takwimu halisi.
Dkt. Wanga alisisitiza kuwa ili kuongeza ushindani wa kibiashara, ni muhimu kila kiwanda kiwe na makao yake makuu ndani ya mkoa kilipo.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani (TCCIA), Said Mfinanga, aliomba gharama za upatikanaji wa ardhi kwa wafanyabiashara wazawa zipunguzwe.
Aidha, alimpongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Pwani kwa kuvuka lengo la ukusanyaji kodi kwa asilimia 100, huku akieleza kuwa walipa kodi wameongezeka kutoka 27,154 mwaka 2024 hadi 28,735 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 10.

