Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa kiasi cha shilingi bilioni 42.34 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha ili kumaliza migogoro ya ardhi na uendelezaji wa maeneo mbalimbali katika mkoa huo.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Moshono, Jijini Arusha, Makonda amesema fidia hiyo imetolewa kwa maeneo kadhaa yaliyoguswa na miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, uwanja wa ndege, maeneo ya jeshi, na uchimbaji wa madini.

Katika Jiji la Arusha, eneo la Losirwa lililokuwa chini ya matumizi ya Jeshi limepewa fidia ya shilingi Bilioni 2.27, ambapo fidia hiyo imekwishalipwa, eneo la Oloresho kwaajili ya maandalizi ya mashindano ya AFCON, limetengewa fidia ya shilingi bilioni 7.27,  barabara ya Mianzini – Ngaramtoni nayo imelipwa fidia ya shilingi bilioni 3.49 ambapo fedha hizo zimelipwa tayari pamoja na eneo la barabara ya Mirongoine – Olmot limepokea fidia ya shilingi milioni 591.64 ambayo nayo imelipwa.

Aidha, Wilaya ya Arumeru, fidia kwa eneo la Jeshi lililopo Duluti imetolewa kwa kiasi cha shilingi bilioni 7.9 na tayari imelipwa yote kwa walengwa.

Wilaya ya Karatu imepata fidia ya shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya uwanja wa ndege wa Manyara uliopo katika eneo hilo, hatua inayolenga kufanikisha uboreshaji wa miundombinu ya usafiri wa anga.

Kwa upande wa Wilaya ya Monduli, eneo la Engaruka, ambalo linahusishwa na shughuli za uchimbaji wa madini ya magadi soda, limetengewa fidia ya shilingi bilioni 14.9, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, Makonda amewataka viongozi wote wa Mkoa huo  kuacha mara moja tabia ya kuwaondoa wananchi kwenye maeneo yao bila kuwapa fidia stahiki, akisisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita inalenga haki, usawa na maendeleo ya watu na ndiyo dhamira ya Rais Dkt. Samia katika kulinda haki za wananchi na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya Taifa.