Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Balozi wa shirika la wanaume wanaopitia changamoto dhidi ya unyanyasaji katika ndoa nchini SHIWACHANDO, BI Frolence Mtagoa maarufu mama Kanumba ameiomba Serikali kuunda Wizara ya Wanaume ili kuwanusuru na changamoto mbalimbali za unyanyasaji wanazopitia katika maisha ya ndoa.
Mama Kanumba ametoa kauli hiyo akizungumza na JAMHURI DIGITAL hiki kwa njia ya simu akiwa makao makuu ya shirika mkoani Dar es Salaam ambapo amesema kundi la wanaume limekuwa likikabiliwa na matukio ya ukatili wa aina mbalimbali jambo ambalo halileti taswira nzuri katika jamii.
Amefafanua kwamba wanaume waliowengi wanashindwa kuyaripoti matukio ya unyanyasaji hasa kupigwa, kujeruhiwa kama alivyotolea mfano wa hivi karibuni mwanamke aliyemkata nyeti mume wake huko mkoani Manyara.
Amesema sababu mbalimbali ikiwemo ya kuhofia aibu kuchekwa, wanaume imewapelekea kuwa watu wa kukaa kimya ilihali wanayapitia magumu kwenye ndoa.

Balozi huyo ameongeza kuwa wanaume kukaa kimya bila kuyasema wazi matukio ya kikatili dhidi yao imewaathiri kisaikolojia hivyo juhudi zinahitajika kwa kuunda wizara maalumu kwa wanaume ili kuwasaidia zaidi.
Hata hivyo ametoa wito akiwasihi wanawake na wanaume kuishi kwa kuzingatia misingi ya ndoa kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana jambo ambalo litaweza kuleta usawa na hali ya utulivu katika familia.
Naye Elenest Komba Mwenyekiti wa Shirika hilo la SHIWACHANDO na Rais wa Wanaume wanaopigwa na wake zao amesema Novemba 19, 2025 ilikuwa siku ya Maadhimisho ya Wanaume Duniani hivyo kama shirika waliadhimisha kwa kutoa elimu kupitia kauli mbili ikiwemo ya ‘Mwanaume Anahitaji Kudekezwa na Siyo Kunyanyaswa’.
Komba amefafanua kwamba ni matukio mengi yanayojitokeza yakihusisha ugomvi tofatitl tofauti japo imekuwa changamoto kuripotiwa hivyo ameendelea kutoa wito akiwasihi wanaume na wanawake kutoa taarifa ya ukatili pindi inapotokea ili kupata msaada zaidi, kukaa kimya imekuwa ni changamoto kubwa inayochochea ukatili na unyanyasaji kwa jamii.


