Mjane wa Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Maria Nyerere amepokea nishani ya heshima kutoka Jamhuri ya Angola ya kutambua mchango wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika harakati za ukombozi na upatikanaji wa amani nchini Angola.
Akikabidhi nishani hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amesema kuwa Nishani ni heshima kubwa kwa Mwalimu Nyerere na nchi yetu kwa ujumla kutokana na mchango wake kwenye harakati za ukombozi ambapo ardhi ya Tanzania ilitumika kwa ajili ya kutoa hifadhi, kuandaa mipango na mikakati pamoja na mafunzo kwa wapigania uhuru wa mataifa mbalimbali, ikiwemo Angola.
Naye Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Domingos de Almeida da Silva Coelho aliyeungana na Mhe. Kombo kuikabidhi nishani hiyo kwa Mjane wa Baba wa Taifa alisema “Angola inatambua mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika harakati za uhuru wetu. Nishani hii ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru wa Angola na uthibitisho wa mshikamano wa kweli wa Afrika.”
Kwa upande wake Mama Maria Nyerere ameishukukuru Angola kwa nishani hiyo kubwa ya heshima kama alama ya kutambua mchango wa Hayati mumewe akiongeza kuwa juhudi na jitihada za kuikomboa Afrika za Mwalimu Nyerere zisingeweza kuzaa matunda bila ushirikiano mzuri na mshikamano alioupata kutoka kwa viongozi wenzake wengine wa Afrika.

Akishukuru kwa niaba ya familia, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere amesema kuwa Mwalimu Nyerere aliona Tanzania haipo huru hadi nchi zingine za Afrika ziwe huru hivyo aliamua kusaidia na wengine. “Tunashukuru kwa heshima hii kubwa na hata tunapokuja nchini kwenu mnatupokea kwa heshima kubwa mno tunashukuru sana.”
Mwalimu Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi wa Umoja wa Nchi za Afrika za Afrika (OAU), hivi sasa Umoja wa Afrika, kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1985. Nchi zingine zilizonufaika na jitihada hizo ni pamoja na Namibia, Msumbiji, Afrika Kusini, Zimbabwe, Guinea-Bissau na Cape Verde.






