Mameya kadhaa wa eneo la Los Angeles wameungana pamoja kuutaka utawala wa Trump kusimamisha uvamizi dhidi ya wahamiaji ambao umeleta wasiwasi na kuchochea maandamano kote nchini Marekani.
Mameya hao wakiwa na wajumbe wa mabaraza ya miji walimtaka Trump siku ya Jumatano (Juni 11) aache kutumia jeshi pamoja na mawakala wa uhamiaji kwenye msako wake kwa wahamiaji.
Meya wa Los Angeles, Karen Bass, alisema uvamizi huo umezusha fadhaa kubwa ili tu kuiridhisha Ikulu ya White House.
Nakuomba Rais Trump, na tafadhali nisikilize, wacha kabisa kuwatisha wakaazi wetu. Unapaswa kuachana na uvamizi huu.” Alisema Naibu Meya wa Paramount, Brenda Olmos, ambaye mwenyewe alipigwa kwa risasi ya mpira, akizungumza na waandishi wa habari.
Sehemu ya mitaa ya mji huo ilianza utekelezaji wa amri ya kutotoka nje usiku wa Jumanne, lakini eneo linalohusika lina ukubwa wa maili moja tu ya mraba, ilhali mji wenyewe mzima una mailli 500 za mraba.
