Mamia ya wanachama na wafuasi wa chama cha ACT Wazalendo wamempokea Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman, alipowasili katika Uwanja wa Ndege kisiwani Pemba.

Wanachama hao walikuwa wakiimba nyimbo za hamasa na mshikamano, wakiahidi kutorudi nyuma katika mapambano ya kudai haki yao ya kidemokrasia.

Mhe. Othman Masoud aliwasili Pemba akiambatana na mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, ambapo anatarajiwa kuwepo kisiwani humo kwa ajili ya mapumziko maalum pamoja na kutembelea ndugu na jamaa zake.

Akizungumza kwa ufupi na wafuasi hao wakati wa kuwasalimu, Othman alisema hamasa na mshikamano wao ni ishara ya uimara wa chama hicho, akidai hali hiyo “inakitia hofu” Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 “Jamani, kwa wingi wenu na furaha zenu mtawatia homa CCM. Licha ya yote waliyoyafanya, bado mko imara sana,” alisema Othman.

Kihistoria, kisiwa cha Pemba kimeendelea kutambulika kama ngome ya siasa za upinzani, hususan ACT WAZALENDO, licha ya hila na changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika chaguzi mbalimbali.