Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kuwa imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 9,689.833 za dawa za kulevya, pikipiki 11 na magari matatu, kufuatia operesheni maalum zilizofanyika mwishoni mwa Desemba, 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 66 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara, usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya, hatua inayodhihirisha kuendelea kwa mapambano makali dhidi ya uhalifu huo nchini.
Akieleza kuhusu baadhi ya operesheni hizo, mamlaka hiyo imesema kuwa katika eneo la Sinza C, mtaa wa Bustani, nyumba namba 16 jijini Dar es Salaam, ilimkamata Jefferson Kilonzo Mwende (35), raia wa Kenya, akiwa na gramu 131.88 za heroin. Mwende, ambaye amekuwa akiishi Tanzania tangu mwaka 2023, alitumia biashara ya kuuza chai kama njia ya kuficha shughuli zake haramu za dawa za kulevya.
Katika tukio jingine lililotokea mtaa wa Wailes, Temeke, Dar es Salaam, mamlaka ilikamata pakiti 20 za dawa za kulevya aina ya skanka zenye uzito wa kilogramu 20.03, zilizokuwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba na kusafirishwa kwa basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours lenye namba za usajili AAM 297 CA kutoka Msumbiji. Basi hilo hufanya safari zake kati ya Nampula nchini Msumbiji na Tanzania. Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza, Dar es Salaam na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji.
Aidha, katika eneo la Kinyerezi, mtaa wa Majoka wilayani Ilala, watuhumiwa watatu ambao ni Erick Emest Ndagwa (32), Paul Blass Henry (34) na Tido Emmanuel Mkude (35) walikamatwa wakiwa na bangi kilogramu 193.66, zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.
Mamlaka pia ilifanikiwa kukamata pakiti 20 za dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu 9.54, baada ya ukaguzi uliofanyika katika kampuni za usafirishaji wa mizigo jijini Dar es Salaam. Mirungi hiyo ilikuwa imefungwa kwa njia ya kufanana na majani ya mwarobaini yaliyokaushwa, ikisafirishwa kutoka Kenya kuelekea nchini Australia.
Vilevile, kupitia operesheni zilizofanyika katika mikoa ya Mwanza, Sinyanga, Morogoro, Tanga, Lindi, Kilimanjaro, Njombe, Kigoma na Arusha, mamlaka ilikamata dawa za kulevya aina ya heroin gramu 37.34, skanka kilogramu 1.015, bangi kilogramu 7,969.98 na mirungi kilogramu 1,363.701, pamoja na kuteketeza ekari 14 za mashamba ya bangi.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za viashiria vya biashara ya dawa za kulevya, pamoja na kuwa makini kuepuka kubeba au kusafirisha mizigo wasiyoifahamu. Mamlaka imesisitiza kuwa itaendelea na operesheni nchi nzima na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote wanaojihusisha na uhalifu wa dawa za kulevya.



