Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia Arusha

SERIKALI imeahidi kuwa katika bajeti ya mwaka huu itazifanyia kazi changamoto za kikodi zinazolalamikiwa na wafanyabiashara na wenye viwanda kama mkakati wa kuendelea kuvutia uwekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi.

Ahadi hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, wakati wa kikao na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) kilichoangalia changamoto za kikodi na mafanikio ya wenye viwanda.

Alisema nia ya serikali ni kuona wafanyabiashara na wenye viwanda wanafanyakazi kwenye mazingira mazuri zaidi yatakayowafanya wazidi kuongeza uzalishaji.

“Serikali inatambua umuhimu wenu kwenye ukuaji wa uchumi kwa hiyo kwenye bajeti ijayo itazingatia sana maombi na ushauri wenu kuhusu masuala mbalimbali ya kikodi, sote tunajenga nyumba moja” alisema

“Kama mlivyofanya mwaka jana, mwaka huu pia mmetuletea mapendekezo mengine na yale ya mwaka jana kwa asilimia zaidi ya 60 serikali iliyafanyia kazi hii inaonyesha ni jinsi gani ninyi mlivyowashauri wazuri sana wa serikali,” alisema

Alisema Rais Samia anania ya kukuza uwekezaji kutoka nje na ndani ya nchi kwa kuhakikisha kunakuwa na viwanda vingi zaidi na ndiyosababu serikali inajitahidi kuondoa changamoto zote za kikodi.

“Tumesikia changamoto zenu nyingi zinahusu kodi za bidhaa kodi za VAT, sasa tunakwenda kuwasilisha bajeti ya serikali ambapo mambo mengi mliyoshauri tutayagusia, kuna kodi zitaondolewa, kodi zingine zitapunguzwa tutatengeneza bajeti bora kwa ustawi wa viwanda na ninaamini mtatabasamu,” alisema

“Tutahakikisha tunafanya kitu kizuri mpaka mtabasamu kwasababu serikali inawapenda, Rais Samaia anawapenda wawekezaji na wenye viwanda ndiyo maana kila siku anatatua changamoto zenu,” alisema Naibu Waziri

Mkurugenzi Mkuu wa (CTI), Leodegar Tenga alisema mkutano huo ulikuwa muhimu kwaajili ya kuzungumza masuala ambayo yatawasaidia wenye viwanda kuongeza uzalishaji wa bidhaa hususan masuala ya kikodi.

Aliwapongeza manaibu waziri walioshiriki mkutano huo wa wenye viwanda na kuongeza kuwa serikali siku zote imekuwa sikivu kwa wenye viwanda na imekuwa ikizifanyia kazi changamoto zao na kuweka mazingora bora.

“Tumejadiliana masuala ya kikodi na yale ambayo si ya kikodi, tumejadili mambo mengi sana ambayo tunaona dhahiri yatasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa wenye viwanda na kuviwezesha kufanya vizuri zaidi,”alisema Tenga

Alisema moja ya changamoto ya kikodi inayolalamikiwa na wafanyabiashara ni kodi asilimia tisa iliyoanzishwa karibuni na bandari kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ambayo wanasema ni kubwa sana kulinganisha na uhalisia wa biashara.

“Wafanyabiashara na wenye viwanda wanapenda kulipa kodi kwa hiyari lakini wanasema hiyo asilimia tisa ni kubwa mno angalau ingekuwa asilimia mbili au tatu,” alisema

“Bandarini wamesema ukileta mzigo wowote ambao ni hatari unapewa siku moja tu ya kuuondoa ukikaa siku ya pili na kuendelea wananza kukutoza pesa sasa haiwezekani mzigo ukaja leo ukaondolewa leoleo ni ngumu sana hii kwa wafanyabiashara,” alisema

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Deniss Londo alisema amefurahi kusikia wafanyabiashara na wenye viwanda wakisifu uwekezaji uliofanywa na serikali kwenye miundombinu hali inayowasaidia kwenye usafirishaji wa bidhaa wanazozalisha.

Alisema serikali inawatambua wenye viwanda na wafanyabiashara kama wadau wa kimkakati katika kufanikisha Dira ya Taifa ya 2050 na kwamba serikali itaendelea kuwasikiliza ili kuwawekea mazingira bira zaidi ya uzalishaji.