Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imeendeleza juhudi za kuimarisha elimu jumuishi kwa kumwezesha mwanafunzi mwenye ulemavu kupata baiskeli maalum, hatua inayolenga kumrahisishia safari ya masomo na kumsaidia kufikia ndoto zake za kielimu.
Katika muendelezo wa juhudi hizo, Manispaa hiyo imemkabidhi baiskeli kijana mwenye ulemavu, Goodlack Mchome, mkazi wa Kata ya Kibaha Mwendapole na mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Tumbi.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, ambapo Mkurugenzi wa Manispaa, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alimkabidhi rasmi baiskeli hiyo ili kumwezesha kufika shuleni kwa urahisi na kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Dkt. Shemwelekwa alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya elimu bila vikwazo.
Alibainisha kuwa baiskeli hiyo itamsaidia mwanafunzi huyo kufika shuleni kwa wakati, kupunguza changamoto za usafiri na kuongeza ari ya kujifunza, hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa akipitia mazingira magumu ya kufika darasani.
“Moja ya vipaumbele vya Serikali ni utekelezaji wa elimu bila malipo na kuondoa changamoto zinazoweza kumzuia mtoto kupata elimu ya msingi”
” Tutaendelea kuhakikisha baiskeli hii inakuwa katika hali bora, Ikiharibika muda wowote, tutaitengeneza ili kuhakikisha Goodlack anaendelea kupata elimu bila kikwazo chochote,” alielezea Dkt. Shemwelekwa.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Jaqueline Mbwambo, aliishukuru Manispaa ya Kibaha kwa msaada huo, akisema umeondoa changamoto kubwa ya usafiri iliyokuwa ikimkabili mwanawe.
“Namshukuru sana Rais Samia na Manispaa ya Kibaha kwa kutatua changamoto ya usafiri iliyokuwa ikimzuia mwanangu kwenda shule kwa wakati, Sasa ataweza kusoma kwa amani na kufikia ndoto zake,” alisema Jaqueline.
Hatua hii inaendelea kuonesha dhamira ya Manispaa ya Kibaha katika kuboresha maisha ya watu wenye mahitaji maalum na kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika safari ya elimu.



