Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mwaka 2026 imejenga na kufungua shule mpya za awali na msingi za mchepuo wa Kiingereza, hatua inayolenga kukidhi mahitaji ya wananchi waliokuwa wakihitaji huduma hiyo kwa gharama nafuu.

Miongoni mwa shule hizo ni Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu, ambayo tayari imekamilika kwa gharama ya sh. Milioni 569,264,013.76 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri, ikiwa na madarasa ya kisasa, madawati, vyoo na walimu wa kutosha.

Aidha, Shule ya Msingi Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi ambapo hadi sasa, jumla ya sh. Milioni 252,897,072.40 tayari zimekwishatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, huku milioni 151,760,000.00 zikitarajiwa kutolewa ili kukamilisha ujenzi wake.

Akizungumza kuhusu miradi hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Shemwelekwa alisema uanzishwaji wa shule hizo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora katika mazingira rafiki .

Alisisitiza , Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi hadi kukamilika kwa Shule ya Msingi Mwambisi ili ianze kutoa huduma kama ilivyopangwa.

Shemwelekwa alitoa wito kwa jamii kushirikiana na Serikali katika kulinda na kudumisha miundombinu ya shule hizo ili iwe na manufaa ya muda mrefu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Baadhi ya wakazi Kibaha akiwemo Zulha Muhammed aliipongeza Manispaa hiyo kwa juhudi na mipango inayolenga kuboresha upatikanaji wa elimu ya mchepuo wa Kiingereza, bila kuwalazimu wazazi kugharamia ada kubwa katika shule binafsi.