Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

MARAFIKI wa Tanzania kutoka nchini Italia (Amici Della Tanzania) wametoa msaada wa vifaa vya elimu na kuboresha vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kipalapala iliyoko katika kata ya Itetemia Mjini Tabora.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni Kompyuta mpakato (laptops) 10 zenye thamani ya sh milioni 6, upakaji rangi vyumba vya madarasa na ofisi za walimu na kuweka umeme katika shule hiyo, vyote vitagharimu zaidi ya sh milioni 10.

Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo baada ya kukabidhi vifaa hivyo jana, Mwenyekiti wa Amici Della Tanzania Epiphana Lubangula kutoka nchini Italia amesema kuwa wametoa msaada huo ili kuboresha miundombinu ya shule hiyo na mazingira ya kijifunzia watoto.

Amebainisha kuwa vifaa hivyo vitasaidia watoto wa shule hiyo kusoma kwa bidii na watakapomaliza shule ya msingi na kuendelea sekondari wawe na uwezo mkubwa wa kutumia komputa (tarakirishi).

Mbali na vifaa hivyo Lubangula amesema kuwa pia wanagharamia upakaji rangi kwenye vyumba vya madarasa vyote, ofisi za walimu na wataleta umeme katika shule hiyo ili kuwezesha watoto kusoma katika mazingira bora zaidi.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya mtoto ni maendeleo ya nchi nzima hivyo mtoto akisomea mahali pazuri atasoma kwa bidii na kuwa na ufaulu mzuri katika mitihani yake ya mwisho na hatimaye aweze kutimiza ndoto zake.

‘Mimi nimezaliwa hapa Kipalapala, hivyo nimekuja kutoa fadhila katika shule yetu, tunataka shule hii ipendeze na iwe na maendeleo makubwa na watoto wasome kwa bidii ili wafike mbali na kusaidia wazazi wao’, amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Mtemi Msagata Fundikira (Mtemi wa Unyanyembe) ameishukuru Familia ya Lubangula kwa msaada waliotoa kwa shule hiyo na kuomba wadau wengine kuiga mfano huo.

Ameeleza kuwa msaada waliotoa kwa shule hiyo ni chachu kubwa kwa maendeleo ya shule hiyo kwani miundombinu yake hususani vyumba vya madarasa, ofisi na sakafu vimechakaa sana na haina umeme pia.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Masumbuko Muyonga amemshukuru dada Epiphana Lubangula na wenzake kwa moyo wao wa upendo kwa shule hiyo, aliahidi kuwa watatumia vizuri komputa hizo na kutunza vizuri miundombinu.

Aidha ameeleza kufurahishwa na msaada wa Taasisi hiyo wa kuwaletea umeme kwani utakapofika utawarahisishia utekelezaji majukumu yao ikiwemo kutumia komputa walizopewa kuchapa taarifa za wanafunzi na kuandaa mitihani.