MAAFISA wa Marekani na China wanatazamiwa kuanza mazungumzo wiki hii ili kujaribu kupunguza vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.

Naibu Waziri Mkuu wa China He Lifeng atahudhuria mazungumzo hayo nchini Uswizi kuanzia tarehe 9 hadi 12 Mei, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema.

Waziri wa Hazina ya Marekani Scott Bessent na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani (USTR) Jamieson Greer watawakilisha Washington katika mkutano huo, ofisi zao zilitangaza.

Tangu arejee katika Ikulu ya White House, Rais Donald Trump ametoza ushuru mpya wa kuagiza bidhaa za China hadi 145%.

Beijing imelipiza kwa ushuru 125% kwa baadhi ya bidhaa kutoka Marekani.

Lakini wataalamu wa biashara duniani wameiambia BBC kwamba wanatarajia mazungumzo kuchukua miezi kadhaa.

Vyombo vya habari vya serikali ya China viliripoti kuwa Beijing imeamua kushirikiana na Marekani baada ya kuzingatia kikamilifu matarajio ya kimataifa, maslahi ya nchi na maombi kutoka kwa biashara za Marekani.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa China iko tayari kwa mazungumzo lakini ikasisitiza kuwa ikiwa nchi hiyo itaamua kuendelea kupigana vita hivi vya kibiashara, itapigana hadi mwisho.

Vita vya kibiashara vimezua msukosuko katika masoko ya fedha na kusababisha mitikisiko katika biashara ya kimataifa.