Maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi kutoka Marekani na mataifa ya Ulaya wamekutana kwa mara ya kwanza mjini Washington kuandaa mipango ya utekelezaji wa mkataba wa amani kati ya Urusi na Ukraine pindi utaafikiwa.

Mkutano huo umejumuisha maandalizi ya kijeshi na namna ya kuilinda Ukraine kufuatia ahadi ya nchi za magharibi ya hakikisho la usalama wa muda kwa nchi hiyo baada ya vita.

Hata hivyo Rais Donald Trump wa Marekani ambaye siku ya Jumatatu aliunga mkono kuipatia Ukraine dhamana ya usalama amesema nchi yake haitotuma vikosi vya ardhini na badala yake huenda itatoa ulinzi wa anga.

Nchi kadha za Ulaya zimesema ziko tayari kuchangia wanajeshi watakaokuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa mkataba wowote wa amani utakaopatikana kati ya Urusi na Ukraine. CHANZO DW