Ikulu ya Marekani imemfuta kazi Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), Dkt. Susan Monarez, baada ya kukataa kujiuzulu siku ya Jumatano.

Kupitia taarifa rasmi, Ikulu ilieleza kuwa Dkt. Monarez “hailingani na ajenda ya rais,” na kwa sababu hiyo akaondolewa rasmi katika nafasi yake katika taasisi hiyo ya afya ya umma.

Hapo awali, Idara ya Afya ya Marekani ilikuwa imetangaza kuondoka kwake, hali iliyosababisha majibu kutoka kwa mawakili wa Dkt. Monarez waliodai kuwa hakujulishwa kuhusu hatua hiyo na kwamba hakuwa na nia ya kujiuzulu.

Mawakili wake walidai kuwa mteja wao alikuwa akilengwa kwa sababu ya kukataa “kupitisha maagizo yasiyo ya kisayansi na ya hatari, na kufukuza wataalamu wa afya waliobobea,” huku wakimtuhumu Waziri wa Afya, Robert F. Kennedy Jr., kwa “kutumia afya ya umma kama silaha ya kisiasa.”

“Kama ilivyoelezwa wazi katika tamko la mawakili wake, Susan Monarez hailingani na ajenda ya rais,” Ikulu ilisisitiza baadaye Jumatano, ikiongeza kuwa amefutwa kazi rasmi kama mkurugenzi wa CDC.

Dkt. Monarez, mwanasayansi mwenye uzoefu wa muda mrefu katika serikali ya shirikisho, aliteuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump kuongoza CDC, na uteuzi wake ulithibitishwa na Seneti kwa kura zilizogawanyika kisiasa mnamo Julai.

Uteuzi wake ulifuatia hatua ya Trump ya kuondoa uteuzi wa awali wa aliyekuwa Mbunge wa Republican, Dave Weldon, ambaye alikumbwa na upinzani kutokana na misimamo yake kuhusu chanjo na uhusiano wake na ugonjwa wa usonji (autism).

Kuondolewa kwa Dkt. Monarez kunajiri takriban wiki moja baada ya chama cha wafanyakazi wa CDC kutangaza kuwa wafanyakazi wapatao 600 walifutwa kazi.

Mabadiliko hayo makubwa yamewaathiri wafanyakazi waliokuwa wakihusika na agenda ya serikali dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kama mafua ya ndege, pamoja na watafiti wa hatari za kimazingira na wale waliokuwa wakishughulikia maombi ya taarifa za umma.