Hatimaye, Marekani imeingia rasmi katika mgogoro wa kijeshi kati ya Israel na Iran kwa kuishambulia Iran moja kwa moja, katika kile kinachoelezwa kuwa ni hatua ya kuisaidia Israel katika vita vinavyoendelea kwa zaidi ya siku kumi. Kwa kutumia ndege za kivita za kisasa aina ya B-2, Marekani imeshambulia vinu vitatu vya nyuklia vya Iran vilivyopo Natanz, Fordow na Isfahan.
Hata hivyo, taarifa kutoka Tehran na Moscow zinadai kuwa Iran ilishahamisha vifaa muhimu kutoka katika vinu hivyo kabla ya shambulio hilo kufanyika. Kwa mujibu wa taarifa rasmi za pande zote, hakuna madhara ya vifo wala mionzi iliyoripotiwa katika maeneo hayo, jambo linalodokeza maandalizi ya awali na tahadhari kutoka kwa Iran.
Shambulizi hili limetajwa kuwa kubwa na lenye athari za kimkakati dhidi ya Iran na washirika wake wakuu, hasa Urusi na China. Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema kuwa lengo la Marekani ni kuilazimisha Tehran kusitisha mradi wake wa kurutubisha uranium, unaotajwa kuwa na malengo ya kutengeneza silaha za nyuklia.
Mara baada ya mashambulizi hayo, Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, alilihutubia taifa akionya Iran dhidi ya kujibu mashambulizi hayo kwa kushambulia kambi za kijeshi za Marekani au Israel. Alisisitiza kuwa Iran haina budi kuingia kwenye meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wa Israel, Waziri Mkuu wake ambaye katika siku za awali za vita hizi alionekana kupoteza uungwaji mkono wa kisiasa na kijamii ndani ya Tel Aviv, alitokea mbele ya vyombo vya habari na kuishukuru Marekani kwa msaada mkubwa. Katika hotuba yenye maelezo ya kina na sifa tele kwa Trump, alienda mbali hadi kumtangaza kuwa ndiye kiongozi bora duniani, kwa kiwango kinachoonekana hata kuzidi kile kinachoonyeshwa na baadhi ya wafuasi wa Republican nchini Marekani.
Kwa upande wa Iran, Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei alilaani vikali mashambulizi hayo na kuyataja kuwa ni uchokozi wa wazi dhidi ya taifa huru. Akiwa mafichoni kwenye mahandaki, Ayatollah ameapa kuwa Iran itajibu mashambulizi hayo kwa hatua kali ambazo Marekani haitawasahau. Katika kuonesha umakini wake, alithibitisha kuwa tayari ameshateua mrithi wa nafasi yake iwapo atauawa, ingawa hakulitaja jina hadharani. Inaelezwa kuwa mrithi huyo huenda akawa mmoja wa viongozi wa kidini au wa kijeshi ndani ya Kikosi cha Mapinduzi cha Iran (IRG).
Vinu vya nyuklia vilivyoshambuliwa vinatajwa kuwa katika maeneo ya ulinzi mkali ardhini, hadi kufikia mita 300 chini ya ardhi. Hata hivyo, Iran bado ina vinu vingine vitano muhimu vya nyuklia: Arak, Ardakan, Yazd, Bushehr na Karoon. Pia kuna vituo maalum vitatu vya “nuclear reactors” vilivyopo Bonab, Tehran na Ramsar, pamoja na migodi mikuu ya uranium ya Sanghand, Narigan na Gachin. Kambi ya kijeshi ya Parchin pia inatajwa kama kitovu cha shughuli za kijeshi za nyuklia nchini humo.
Kwa upande wa washirika wa Iran, bado Moscow haijatoa kauli rasmi kufuatia mashambulizi haya, ingawa siku chache zilizopita ilitoa onyo kali kwamba jaribio lolote la kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran litakuwa kichocheo cha kuingiza dunia kwenye vita vya tatu vya dunia.
Kwa sasa, dunia inasubiri kwa taharuki kuona ni nini kitafuata baada ya hatua hii hatari kutoka kwa Marekani. Je, Iran itajibu kwa nguvu kama ilivyoapa, au itaamua kukaa kwenye meza ya mazungumzo? Na je, Urusi na China watasimama kwa vitendo kuilinda mshirika wao, au wataendelea kuwa watazamaji? Majibu ya maswali haya yataamua mustakabali wa amani au mtafaruku wa dunia.
