Marekani kwa mara nyingine imeitishia serikali ya Iran juu ya uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi kutokana na ukandamizaji wakati wa maandamano makubwa ya kitaifa.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema rais wa Marekani Donald Trump ni “mtu wa vitendo,” si wa maneno yasiyoisha kama wanavyoona katika Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wake Naibu Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Gholamhossein Darzi, amesema Tehran haitafuti kuongeza mvutano.
“Iran haitafuti kuongeza mvutano wala makabiliano. Hata hivyo, kitendo chochote cha uchokozi, cha moja kwa moja au kisicho cha moja kwa moja, kitajibiwa kwa hatua madhubuti, inayowiana na sheria, chini ya Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”
“Hili si tishio, bali ni kauli ya uhalisia wa sheria. Uwajibikaji wa madhara yote utakuwa juu ya wale watakaoanzisha vitendo hivyo haramu.”
Tangu kuanza kwa maandamano makubwa dhidi ya utawala wa kiimla katika Jamhuri ya Kiislamu zaidi ya wiki mbili zilizopita, Trump ametishia mara kadhaa kuingilia kati Iran kwa nguvu za kijeshi.


