Marekani imesema imeyashambulia maeneo zaidi ya 90 ya kijeshi ya Iran katika kisiwa cha Kharg, huku Iran nayo ikijibu mashambulizi hayo kwa kufyetua makombora na droni kuelekea Israel na katika nchi jirani za Ghuba.

Kamandi kuu ya jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema kuwa vikosi vyake vimefanya shambulio kubwa katika Kisiwa cha Kharg nchini Iran Ijumaa usiku na kufanikiwa kuyalenga maeneo zaidi ya 90 ya kijeshi ya Tehran.

Rais Donald Trump amesema vikosi vya Marekani “vimeangamiza” maeneo ya kijeshi kwenye Kisiwa hicho ambacho ni makao makuu ya kituo kinachoshughulikia usafirishaji wa mafuta nchini humo. Spika wa bunge la Iran alikuwa ameonya kwamba mashambulizi kama hayo yangesababisha hatua mpya na kubwa ya kulipiza kisasi.

Wakati huo huo, afisa mmoja wa Marekani amesema wanajeshi 2,500 wa ziada pamoja na meli ya kivita wanatumwa katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwa ni takriban wiki mbili tangu kuanza kwa vita hivyo vya Marekani na Israeli dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakati Israel ikiendeleza pia mashambulizi huko Lebanon, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema siku ya Jumamosi kuwa serikali ya Beirut iko tayari kufanya “mazungumzo ya moja kwa moja” na Israel ili kusitisha mapigano na akapendekeza kuandaa mkutano utakaozikutanisha pande hizo mbili mjini Paris.